Wakaguzi wa Mazingira Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Pwani, Tanga na Morogoro wametakiwa kujikita katika kutoa ushauri wa Kitaalamu juu ya suala nzima la uharibifu wa mazingira badala ya kufikiria zaidi kutoa adhabu.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Clifford Tandari wakati akifungua mafunzo ya wakaguzi wa mazingira Mikoa ya Morogoro, Tanga na Pwani yaliyofanyika chuo kikuu cha sokoine, Mjini Morogoro.
Dkt. Kebwe amesema pamoja na kuwa Wakaguzi hao wana kazi ngumu na inayohitaji umakini lakini pia Wakaguzi hao (environmental inspectors) wametakiwa kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa ikiwa ni pamoja na kukjikita katika kutoa ushauri zaidi pindi wanapoona kuna uvunjifu wa sheria za mazingira na kwamba hatarajii kusikia wanatoa adhabu, bila kwanza kutoa ushauri wa kitaalam. Alisema Dkt. Kebwe.
Aidha, Dkt. Kebwe amesema Viongozi wa Mikoa ya Kanda ya Mashariki wanaamini kuwa kwa Kuteuliwa Wakaguzi hao wa Mazingira na kwa madaraka makubwa waliyopewa na Mhe. Waziri mwenye Dhamana ya Mazingira hawatarajii kuona au kusikia matukio ya uharifu wa mazingira kwenye Mikoa yao na kuwa katika mkoa wa Morogoro hatakubali kusikia uharibifu wa mazingira unatokea katika maeneo ambayo mkaguzi wa mazingira yupo.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amewaasa Wakaguzi hao kuelewa kuwa kwa sasa nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda, hivyo wanatakiwa kuwasaidia wawekezaji kuwekeza na kuzalisha bidhaa bila kuharibu mazingira yaliyopo.
Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo hayo, Mratibu wa Mazingira Kanda ya Mashariki Bw. Japhari Chamgege alisema Wakaguzi wa Mazingira wameteuliwa na Waziri kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Kifungu cha 182 (1) & (2) kinachompa Waziri mwenye dhamana ya Mazingira mamlaka ya kuteua Wakaguzi wa Mazingira miongoni mwa mtumishi kutoka mamlaka za Serikali za mitaa, Wizara au Asasi yoyote ya umma.
Chamgege amesema kutokana na sheria hiyo Mhe. Waziri amekwisha teua Wakaguzi wa Mazingira 471 kote nchini na kufanya idadi ya Wakaguzi hao kufikia 500 ukijumuisha na Wakaguzi wa Mazingira waliokuwepo kabla ya Uteuzi huo.
Aidha, Mratibu huyo wa Mazingira alibainisha majukumu ya Wakaguzi hao wa Mazingira kuwa ni pamoja na kuingia kwenye jengo lolote, ndani ya gari, ndege, chombo cha majini, ardhi au mahali pengine pasipo kuwa na makazi ya kawaida ya watu ili kufanya ukaguzi.
Majukumu mengine ni kusimamisha gari au chombo chochote cha majini au ardhini ambacho wanaamini kwa dhati kuwa chombo hicho kinaendeshwa na kinamwaga au kimekwishamwaga kitu chochote kinachochafua mazingira kinyume cha sheria hii au, kukamata au kuzuia shughuli yeyote inayoharibu mazingira.
Mmoja wa Wakaguzi wa Mazingira Walioteuliwa na Waziri mwenye Dhamana, Bw. Venance Segere ambaye ni Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, amesema anashukuru kwa uteuzi huo kwani unampa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii zaidi kwa kuwa ameaminika na Serikali. Aidha, amesema warsha hiyo imekuja wakati mwafaka kwao na watatumia utaalamu wao na vipaji kwa uaminifu kwa ajili ya kuwasaidia watanzania wenzao ili waweze kuishi katika mazingira bora zaidi.
|
|
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa