Wakazi wa Kijiji cha Chabima kilichopo kata ya Masanze wilayani Kilosa wamekuwa wakitembea umbali wa kilomita 35 tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho ili kuweza kufika hospitali ya wilaya ya Kilosa ili kupata huduma za kiafya.
Hayo yamebainishwa Februari 3 mwaka huu kijiji hapo wakati Kamati ya CCM Wilaya ilipotembelea Mradi wa Mkaa endelevu na ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Chabima ambapo imebainishwa kuwa wakazi wa kijiji hicho hutembea umbali mrefu ili kupata huduma za kiafya jambo lililopelekea kijiji hicho kuazimia kujenga zahanati ili iweze kuwasaidia kupunguza adha yakutopatikana kwa ukaribu kwa huduma hizo.
Akisoma taarifa hiyo mjumbe wa kamati ya maliasili ya kijiji cha chabima Idd Tangula amesema kuwa kijiji hicho kimeanzishwa mwaka 1973 na hakukuwa na zahanati kwa kipindi chote hadi mwaka 2012 ndio ulianza ujenzi wa zahanati inayogharimu milioni 120 ambayo imekamilika kwa nguvu kazi za wananchi,halmashauri ikiwa imetoa milioni 32 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Mh. Ameir Mubarak akitoa mifuko 50 ya saruji na kwamba kwasasa wanamalizia ujenzi wa choo.
Aidha amesema kuwa licha ya kukamilika kwa ujenzi huo bado wanakabiliwa na changamoto ya samani za ofisi, vifaa tiba, bomba la maji na daktari hivyo wameiomba Serikali kuwasaidia ili waweze kuepukana na adha hiyo ambayo inagharimu maisha ya watu hususan wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya Alhaj Majid Mwanga ameonyesha kutoridhishwa na gharama za ujenzi ambazo hazilingani na ubora wa jengo uliopo ambapo imetumika zaidi ya milioni 86 mpaka sasa.
Mwanga licha ya kasoro zilizopo katika ujenzi huo unaoendelea ameitaka Serikali ya kijiji kuhakikisha ujenzi huo unakamilika mara moja na fedha ambayo ipo itumike katika ununuzi wa vitanda vya kujifungulia wazazi ili wananchi waanze kupatiwa matibabu kijijini hapo huku akiahidi kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha daktari anapatikana ujenzi utakapokamilika ambapo pia amewahamasisha wananchi hao kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 kwa kupata chanjo ya Uviko 19.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa