Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yamefanyika leo Agosti 6, 2025 katika viwanja vya Kliniki ya Mama na Mtoto wilayani Kilosa, yakilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na mazingira rafiki kwa mama mnyonyeshaji.
Afisa Lishe wa Wilaya, Jackson Kalibwani, ameeleza kuwa lishe bora kwa mama anayenyonyesha ni nguzo ya kwanza ya kuhakikisha mtoto anapata maziwa ya kutosha na yenye virutubisho muhimu.
Aidha amesisitiza ulaji wa makundi yote sita ya chakula, akibainisha kuwa hali ya lishe duni kwa mama huathiri moja kwa moja ukuaji wa mtoto, pia amewashauri wanafamilia kushirikiana katika kumsaidia mama mnyonyeshaji kimazingira na kihisia.
Naye Mratibu wa huduma za mama na mtoto, Bi. Prisca John amesema kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo ni silaha madhubuti dhidi ya vifo vya watoto wachanga ambapo pia ameeleza umuhimu wa chanjo kwa watoto kama sehemu ya kuhakikisha afya bora, huku akisisitiza wajibu wa wazazi kufuatilia huduma hizo kwa karibu.
Kwa upande wake Mgeni rasmi Odilia Haibei akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, amehimiza ushirikiano wa serikali na wadau kama Compassion na World Vision katika kuhakikisha elimu ya lishe na afya inawafikia wananchi wote, hasa walioko vijijini huku akiwataka wakazi wa Kilosa kutambua kuwa uwekezaji katika lishe na mazingira salama ya unyonyeshaji ni uwekezaji kwa taifa lenye afya na uwezo wa kiuchumi.
Kauli mbiu ya mwaka huu “Thamini Unyonyeshaji; Weka Mazingira Wezeshi kwa Mama na Mtoto” imekuwa kiini cha mafunzo na elimu kwa wakazi wa Kilosa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa