Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Steven Kebwe amewataka wananchi wa kata Madoto Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kuacha kubaguana na badala yake amewataka kudumisha amani na ushirikiano kwa kuzingatia utu na sheria zilizowekwa.
Wito huo umetolewa Septemba 7 mwaka huu wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Madoto uliolengo kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika eneo hilo ambapo wakulima wanawataka wafugaji kuondoka wakidai kuwa kijiji ni cha wakulima.
Dkt. Kebwe amesema kuwa katiba ya nchi inasema kila mtanzania ana haki ya kuishi popote hivyo suala la wakulima kuwataka wafugaji kuondoka katika maeneo hayo si sawa na kwamba jambo la msingi ni kukaa pamoja na kujipanga ili kuona migogoro hiyo inatatuliwa kwa njia zipi na kwa amani.
Amesema kuwa anafahamu fika wananchi wa eneo hilo bado wana majeraha mioyoni mwao kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyotokea mwaka 2000 ambapo baadhi ya watu walipoteza uhai katika kadhia hiyo, hivyo hatarajii mambo hayo yajirudie na ameunda tume ya wataalam kutoka wilayani na mkoani watakao chunguza kiini cha mgogoro huo ili kuupatia ufumbuzi wa kudumu.
Awali akitoa taarifa yake juu ya Mgogoro huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bw. Francis Kaunda amesema kuwa ni kinyume cha sheria kuwafukuza wafugaji na kwamba ni vyema viongozi kuanzia ngazi za chini kuangalia njia zinazotumika kuwaingiza wafugaji wapya katika eneo hilo ili kuona kwa jinsi gani wanaweza kuzirekebisha kwa lengo la kuboresha zaidi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa