Mkuu wa Wilaya ya Kilosa adam mgoyi ameitaka jamii ya wakulima na wafugaji kuwa na hulka ya maridhiano hasa katika matumizi ya ardhi kwani kila mtu anayo haki ya kuishi na kutumia ardhi kwa kufuata taratibu na kutenga maeneo kwa kadri ya matumizi kulingana na shughuli zao kwani jamii zote mbili ni watanzania ambao wana haki ya kufanya shughuli zao kwa uhuru kwa kufuata taratibu.
Mgoyi amesema hayo Machi 26 mwaka huu alipotembelea kijiji cha Mfulu yalipotokea mauti ya mkulima ambapo amesema kuwa watendaji wa kata wanao wajibu wa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kupanga maeneo kwa matumizi mazuri na kuhakikisha lazima kuwepo na njia kwa ajili ya kupita mifugo badala ya kulima maeneo yote kwani kutokuwepo kwa njia za mifugo kutasababisha migogoro ikiwemo mapigano ya wakulima na wafugaji.
Akizungumzia kuhusu kifo cha mwanamke aliyefariki maeneo hayo Mkuu wa Wilaya amesema hadi sasa chanzo cha kifo cha mama huyo bado hakijafahamika na kwamba hatua zilizochukuliwa baada ya tukio hilo ni kuupeleka mwili wa mama huyo hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya uchunguzi, hivyo amewataka wananchi hao kuwa watulivu mpaka hapo taarifa za uchunguzi wa kidaktari zitakapotolewa kubainisha chanzo cha kifo hicho.
Aidha mgoyi amesema kwa sasa hakuna kijiji cha Mabwegere kwa mujibu ripoti iliyotolewa na mchunguzi kwani hati ya awali iliyotolewa kwa kijiji hicho iligubikwa na dhuluma na kwamba kwa sasa mwenye mali kwa eneo hilo ni Mkurugenzi Mtendaji na kwamba eneo hilo litatambulika rasmi mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote za uchorwaji upya wa ramani kwani kwa sasa ramani ya iliyokuwa Mabwegere haitambuliki mpaka hapo vijiji vitakapotengwa upya kwa kufuata taratibu ambapo kwa sasa eneo hilo liko chini ya kijiji mama cha Mfulu.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi Daud Nkuba amesema kuwa baada ya kupata taarifa walifika eneo la tukio wakiwa wameambatana na daktari na kufanya uchunguzi wa awali kujua chanzo cha tatizo na kwamba kwa upande wa Jeshi la Polisi wamefanya mahojiano na baadhi ya wakazi wa eneo hilo ili kufatilia wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo ambapo inadaiwa kuwa mkulima huyo ajulikanaye kama Asha Shomari (56) mkazi wa Morogoro baada ya kuona ngombe wameingia shambani kwake ambalo mpunga ndio umeanza kuchipua alikimbilia shambani humo kwa lengo la kuzuia ndipo alipokumbwa na umauti.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa