Fursa mbalimbali hujitokeza kutokana na njia mbalimbali ikiwemo changamoto za jamii, kuanzishwa kwa miradi mikubwa katika maeneo jamii inakoishi, kuongezeka kwa idadi ya watu, kuvumbuliwa kwa rasilimali ya asili kama vile madini, gesi nk au kukua kwa uchumi wa jumla ambapo watu huweza kutumia njia hizo kufanya shughuli za kujiongezea kipato kwa njia ya biashara.
MENEJA URASIMISHAJI RASILIMALI ARDHI VIJIJINI ANTHONY TEMU
Hayo yamebainishwa Anthony Temu Meneja Urasimishaji Rasilimali Ardhi Vijijini kutoka MKURABITA wakati wa mafunzo kwa wakulima waliorasimisha ardhi zao na kupata hati miliki katika kijiji cha Magubike katika kata ya Magubike juu ya masuala mbalimbali ya kilimo, uthaminishaji ardhi na ushirika ambapo upande wa kutafuta fursa Temu amesema utafutaji fursa na namna ya kuzitumia jamii inapaswa kuzitambua vema fursa na kuchukua hatua ya uthubutu katika kufanya michakato mbalimbali ili kuboresha kipato na kuinua ufanisi na kujiwezesha kiuchumi kutokana na ujasiliamali kwani ujasiliamali ni kuwa na mshawasha wa kutafuta na kupata mali kwa kutambua fursa mbalimbali za biashara.
DIWANI WA KATA YA MAGUBIKE MH. CHILOLO AKIWA MMOJA YA WASHIRIKI WA MAFUNZO, 2 & 3 BAADHI YA WASHIRIKI WA MAFUNZO HAYO KATIKA KIJIJI CHA MAGUBIKE
Temu amesema jamii inaweza kutambua fursa kupitia mambo makubwa matatu ambayo ni motisha utokanao na kutafuta fursa kwa sababu kuna motisha katika kufanya jambo husika, msukumo na namna gani ya kufikia fursa hizo ambapo amesema mambo mengine ya kuzingatia ni ufuatwaji wa sheria na taratibu za fursa husika, kuzingatia hali halisi ya eneo husika, kuzingatia mwenendo wa maisha ya wakazi wa eneo husika na mfumuko wa bei aidha amesema kuwa fursa zinaweza kutumika kwa kuangalia namna ya upatikanaji wa huduma unayotaka kutoa, idadi ya ushindani wanaotoa huduma husika, matakwa ya wateja katika eneo na idadi yao pamoja na gharama za uendeshaji wa biashara ambapo pia amesema utafutaji wa fursa utaleta maendeleo ya haraka kiuchumi, huku ubunifu ukiongeza shughuli za aina mbalimbali katika jamii na kuongeza ufanisi pamoja na kupanua soko.
MTHAMINI WA ARDHI BW. LIBERATUS AKITOA ELIMU YA UTHAMINISHAJI WA ARDHI
Naye Mthamini toka Idara ya Ardhi Wilaya ya Kilosa Bw. Liberatus Modest amesema kuwa ardhi inaweza kutumika kujiongezea kipato kwa kuiongezea thamani na ulinzi ambao ni hati miliki ambayo inasaidia katika kupata mkopo lakini pia dhamana hivyo watu wanapaswa kufahamu umuhimu wa nyaraka za ardhi na kuzitunza kwani ardhi inapaswa kuongezwa thamani kwa kuzingatia matumizi ya ardhi kwa asilimia kubwa na kutegemea nyaraka zilizopo zinazozipa ulinzi, pia matumizi ya ardhi yanachangia kwa kiasi kikubwa thamani ya ardhi kuongezeka kutokana na vilivyopo ndani ya ardhi kama vile kupanda mazao ya kibiashara yenye kudumu na ushindani katika soko kama minazi nk lakini pia kujenga nyumba ya kudumu na yenye viwango mfano makazi na biashara.
AFISA USHIRIKA BI ROSE AKITOA ELIMU YA USHIRIKA
Akizungumzia umuhimu wa ushirika Afisa Ushirika Wilaya Rose Matemba amesema kuwa na chama cha ushirika kunawezesha wanaushirika kuwa na uhakika wa mahali pa kukusanyia bidhaa zao wakati wakisubiri bei nzuri ya uhakika wa soko, kutoa fursa inayomwezesha mwanaushirika kushiriki katika uchumi wa jamii anamoishi, kuwawezesha kukopesheka na taasisi mbalimbali za kifedha, kuweza kupata fursa mbalimbali mfano miradi ya kilimo, pamoja na miradi mingineyo lakini pia vyama vya ushirika vinaweza kutumika kama wakala wa kukusanya ushuru.
Naye afisa kutoka benki ya NMB Kilosa Elibariki Mwambashi amewashauri wakulima kuwaza mahali pa kwenda kuuza bidhaa za kabla ya kuanza kuzalisha kwani kitendo cha kufahamu mahali pa kwenda kuuza itasaidia kwa kiasi kikubwa kujua uzalishe kiasi gani jambo linalosaidia kujua hali ya soko na kuepuka hasara zinazoweza kuepukika lakini pia wao kama benki ili kumkopesha mkulima ama kikundi ni lazima mkulima/kikundi kitambue mahali kitakapopeleka bidhaa zake.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa