Wakuu wa Shule za Sekondari pamoja na Maafisa Elimu Kata wametakiwa kusimamia elimu ili kufikia malengo ikiwa ni pamoja na kukuza ufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, la pili na la tatu lakini pia kupunguza kiwango cha wanafunzi wanaofeli.
Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Taaluma kutoka Divisheni ya Elimu Sekondari Millandu Kinyonga wakati akizungumza na wakuu wa shule za sekondari pamoja na Maafisa Elimu Kata katika kikao kazi kilichofanyika 18 Februari, 2025 katika ukumbi wa Mamboya.
Bi. Millandu amefafanua kuwa malengo ya Halmashauri katika upimaji wa kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2025 ni kufuta daraja sifuri na kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayemaliza kidato cha nne anapata cheti lakini pia kupunguza ufaulu wa daraja la nne na kuongeza ufaulu bora yaani daraja I, II, na III.
Aidha ameongeza kuwa pia Halmashauri inalenga kuboresha miundombinu ya ufundishaji ili kuhakikisha kila shule inafikia asilimia 100 ya ufaulu.
Akiwasilisha taarifa ya matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2024, Daniel Kisoso ambaye pia ni Afisa Elimu Taaluma amefafanua kuwa asilimia 79 ya wanafunzi wa kidato cha pili waliopimwa walifaulu ikiwa ni ongezeko la asilimia 02 kulinganisha na matokeo ya upimaji wa mwaka 2023.
Ameongeza kuwa kwa kidato cha nne, wanafunzi 3882 wamefaulu mtihani ikiwa ni sawa na asilimia 90.2 ya waliofanya mtihani na kuongeza kuwa ufaulu huo umepanda kwa asilimia 08 kulinganisha na matokeo ya mtihani wa mwaka 2023 na kuifanya Halmashauri kushika nafasi ya nne Kimkoa.
Katika hatua nyingine, amewapongeza wakuu wa shule ambao shule zao zimefanya vizuri na kuwataka kuziendeleza jitihada hizo huku akiwataka wakuu wa shule ambazo hazikufanya vizuri kuongeza jitihada ili wapate matokeo mazuri katika mitihani inayofuata.
Naye Katibu Msaidizi Tume ya Utumishi wa Walimu Daud Mchillu amewataka wakuu wa shule pamoja na Maafisa Elimu Kata kusimamia nidhamu shuleni ikiwa ni pamoja na kuzuia utoro wa wanafunzi pamoja na walimu ili kuinua taaluma kwani vitendo hivyo huathiri tendo la ufundishaji na ujifunzaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa