Walimu wakuu wa shule za sekondari wameagizwa kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2020 wanaripoti shuleni na kuanza masomo mara moja kwani shule zimeshafunguliwa tangu tarehe 06/01/2020.
Agizo hilo limetolewa Januari 16 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare katika kikao chake na watumishi mbalimbali ambapo amewataka walimu kuhakikisha wanafunzi wanaripoti na kuanza masomo huku akizitaka shule zote zilizopokea pesa kutoka serikalini za kusapoti elimu zihakikishe fedha hizo zinatumika inavyostahiki na kwamba ukaguzi utafanyika ili kuona kama zimetumika katika usahihi lakini pia ametaka kuwepo kwa tathmini ya elimu kila wilaya ambayo itakuwa ijadiliwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
Aidha katika kikao hicho amehoji hatua gani zilizochukuliwa kwa walimu ambao shule zao zimeonyesha kuwa na matokeo mabaya na kushika nafasi za mwisho ambapo pia amesema mwalimu yoyote ambaye hataonyesha mabadiliko katika kupandisha ufaulu anapaswa kuondolewa katika nafasi ya ukuu wa shule huku akiagiza kuondolewa kwa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mabwerebwere ambaye ni miongoni mwa walimu ambao shule zao zimeendelea kuwa na duni katika ufaulishaji wanafunzi ikiwemo shule za sekondari Zombo, Kutukutu, Mabwerebwere na Mikumi.
BAADHI YA WATUMISHI WAKIMSIKILIZA MKUU WA MKOA
Sambamba na hayo amesema kuwa changamoto zilizoko katika shule za msingi na sekondari zitaendelea kutatuliwa lakini pia ametoa rai kwa walimu wakuu kujipima wenyewe utendaji wao wa kazi huku akimwagiza Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari kuwa na mpango wa kuanzisha madarasa ya kidato cha tano na sita kwani shule zilizopo sasa zenye kidato cha tano na sita ni chache pamoja na kuwa na program ya pamoja ya kuongeza ufaulu kwa shule za serikali na binafsi kwa kidato cha tano na sita na kwa kutunga mtihani mmoja ambao utafanywa na wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita kwa mujibu wa madarasa yao.
Pamoja na hayo amewataka waheshimiwa madiwani kuhakikisha wanajishughulisha katika kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari na kwamba diwani yoyote ambaye atakuwa nyuma katika kuleta maendeleo kwenye kata yake atakuwa amepoteza nafasi ya kugombea nafsi hiyo,
Pia ameipongeza shule ya msingi mazinyungu kwa kufaulisha kwa kiwango cha juu katika matokeo ya darasa la saba na amewazawadia shilingi laki mbili ikiwa ni sehemu ya motisha kwa juhudi walizoonyesha huku upande wa chuo cha utabibu ameitaka TANESCO kuhakikisha miundombinu iliyopo katika chuo hicho inakuwa bora ili kuepusha kutokea kwa majanga ya kuungua moto katika mabweni hayo hakujitokezi tena.
BAADHI YA WATENDAJI WA KATA WAKIMSIKILIZA MKUU WA MKOA
Licha ya maagizo hayo Sanare ameonyesha wa kusikitishwa kwake na malalamiko ya wananchi dhidi ya watendaji wa kata na vijiji kwa kutosimamia vema majukumu yao hali inayoonyesha kukosa uwajibikaji, hivyo amewataka maafisa tarafa kuhakikisha wanawasimamia na kwa yoyote atakayebainika kutowajibika katika nafasi yake hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Pia amekemea vitendo vya rushwa vinavyoendelea na kwamba taarifa hizo za rushwa zinaendelea kuchunguzwa na mtumishi yoyote wa umma atakebainika hatasita kumchukulia hatua huku akitoa onyo kwa maafisa ugani kutenda haki wanapofanya tathmini ili kuepusha kutoweka kwa amani.
Aidha ameuagiza uongozi wa Wilaya kuwasimamia wananchi wote bila kusita na kuhakikisha haki inatendeka pasipo kujali jamii zao ambapo amesema licha ya kuwa yeye ni mmasai lakini jamii itambue kuwa yeye si Mkuu wa Mkoa wa wamasai bali Mkuu wa Mkoa wa watu wote wa mkoa wa Morogoro huku akitoa onyo kwa wakulima na wafugaji ambao wamekuwa wakisababisha migogoro kwa kutoa malalamiko ambayo hayana ukweli ndani yake.
Kwa upande wa maswala ya kifedha ametaka watumishi wote wanaodaiwa pesa( defaulters) kuchukuliwa hatua ikiwemo kurudisha pesa zinazodaiwa na amemwagiza OCD kuwakamata mara moja watumishi wanaodaiwa huku akitaka kuhakikiwa mashine zote za kukusanyia mapato za POS kupitia ili zijulikane ziko kwa watu gani na kwamba watumishi wote wanaodaiwa wakamatwe mara moja na kusimamishiwa mishahara yao mpaka watakapolipa madeni.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa