Katika juhudi za kuimarisha sekta ya elimu nchini, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeendesha mafunzo elekezi kwa walimu wapya 74 wa shule za msingi waliopata ajira hivi karibuni.
Mafunzo haya yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, yakilenga kuwajengea uwezo walimu hao kuhusu maadili ya utumishi wa umma na haki zao kama watumishi wa serikali.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ndg. Ayubu Hussein, aliwahimiza walimu hao kuzingatia maadili ya kazi, kuwa waadilifu, na kuwajibika katika majukumu yao ya kila siku. Alisisitiza umuhimu wa walimu kuwa mfano bora kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, akisema: "Walimu ni nguzo muhimu katika jamii; tabia na mwenendo wao huathiri moja kwa moja malezi na maendeleo ya wanafunzi."
Kwa upande wake, Mkaguzi Mwandamizi kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Edward Clement Kyungu, aliwafahamisha walimu hao kuhusu haki na wajibu wao katika mfumo wa hifadhi ya jamii. Alieleza kuwa walimu hao wataanza kuchangia mfuko huo mara tu wanapoanza kazi rasmi, na kwamba michango yao itawasaidia kupata mafao mbalimbali ikiwemo pensheni, mafao ya ulemavu, na mafao ya wategemezi. "Ni muhimu kuelewa kuwa michango yenu ni uwekezaji kwa maisha yenu ya baadaye," alisema Kyungu.
Mafunzo haya pia yalijumuisha mada mbalimbali zinazohusu sheria na kanuni za utumishi wa umma, mbinu bora za ufundishaji, na usimamizi wa rasilimali za shule. Walimu walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kazi zao, hali iliyosaidia kuongeza uelewa na kuondoa sintofahamu.
Walimu wapya walioshiriki mafunzo haya walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa mwanga kuhusu majukumu yao na jinsi ya kuyatekeleza kwa ufanisi. Waliahidi kutumia maarifa waliyopata kuboresha kiwango cha elimu katika shule zao na kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu nchini.Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuhakikisha kuwa walimu wapya wanaingia kazini wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu majukumu yao na jinsi ya kuyatekeleza kwa kuzingatia sheria, kanuni, na maadili ya utumishi wa umma. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa inaendelea kujitahidi kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu bora.”.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa