Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amepongeza benki ya NMB kwa kujali mahitaji ya wafanyakazi kwa kuweka bidhaa zinazokidhi mahitaji ya makundi mbalimbali ya wafanyakazi hususani walimu ambao wamekuwa wakifaidika na mikopo nafuu na kwamba imekuwa msaada mkubwa katika kukidhi mahitaji ya familia na kuwafanya kufanya kazi kwa amani na kuleta tija katika maeneo yao ya kazi.
Shaka ametoa pongezi hizo Agosti 28 mwaka huu wakati wa warsha fupi ya “Mwalimu spesho-Umetufunza Tunakutunza” iliyowakutanisha walimu wakuu wa shule za msingi, wakuu wa shule za sekondari na walimu wa kawaida kutoka shule mbalimbali za Kilosa ambapo ametoa rai kwa walimu kutumia vizuri fursa ya elimu inayotolewa na NMB kujifunza masuala ya kibenki ikiwemo masuala ya amana, mikopo, bima na huduma mbalimbali za kibenki ambazo zitawasaidia kujenga utamadumi wa kuweka akiba ambazo zitawasaidia katika mahitaji na utatuzi wa changamoto za kifedha pindi zinapojitokeza.
Aidha ameitaka benki ya NMB kuendelea kuandaa program mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya watumishi na wananchi kiujumla ili kuwapatia fursa ya kujua huduma zitolewazo na benki pamoja na kubuni bidhaa na huduma za kawaida ambazo mwananchi wa kawaida ataweza kuzimudu.
Pamoja na hayo amewapongeza sana walimu kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kufanya kazi kwa ufanisi na kwamba wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuwaandaa viongozi wa baadae na kwamba serikali itaendelea kuandaa mazingira bora kwa walimu katika kuendelea kutoa huduma bora kwa kuwawekea mazingira rafiki walimu ya kufanyia kazi na kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi katika kuboresha maisha ya watanzania kwa vitendo.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi Kitengo cha Wateja Maalum Queen Kinyamagoha amesema benki ya NMB imeendelea kuja na suluhisho mbalimbali kwa makundi mbalimbali ikiwemo walimu kama njia mojawapo ya kuleta watanzania kwenye mifumo rasmi ya kifedha na kuipatia Serikali mapato kwa kuwafikia watanzania wengi zaidi hivyo kuchangia idadi ya watanzania wanaotumia huduma za kibenki.
Pamoja na hayo kwa niaba ya NMB amesema NMB wataendelea kuja na suluhu bora na nafuu kwa watanzania na kwamba uwajibikiaji wao kwa jamii utabaki kuwa wa viwango vya juu pamoja na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi ya Taifa na wananchi kiujumla.
Nao walimu kwa nyakati tofauti wameishukuru benki ya NMB kwa huduma mbalimbali ikiwemo uwepo wa mikopo yenye riba nafuu inayotolewa kwa watumishi wa makundi mbalimbali kwani imekuwa msaada kwao katika kuwasaidia kujikimu kimaisha na kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali huku wakishukuru kwa elimu inayoendelea kutolewa na benki hiyo ambayo inawasaidia kupata uelewa zaidi juu ya huduma mbalimbali za kifedha.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa