Wakuu wa shule, waratibu elimu kata sambamba na walimu wa lishe katika shule za sekondari wametakiwa kusimamia na kuhakikisha chakula kinachopatikana mashuleni kikiwa katika ubora lakini pia kizingatie makundi matano ya chakula ili kuwasaidia wanafunzi kupata virutubisho vyote badala ya kuagiza vyakula vya aina moja ambavyo havijazingatia ulaji wa mlo kamili kwa wanafunzi.
Rai hiyo imetolewa Septemba 3 mwaka huu na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Bi. Paula Nkane wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo walimu namna ya utoaji wa elimu ya lishe ya vijana balehe kwa kutumia zana za mawasiliano na mabadiliko ya tabia katika vikundi rika ambapo amewataka walimu hao kuhakikisha chakula wanachopewa wanafunzi kiwe kimekamilika ili kuwafanya kuwa na afya bora kwa maisha yao ya baadae.
Paula amesema kuwa walimu wamekuwa wakiagiza vyakula pasipo kuzingatia makundi matano ya vyakula ambapo amewataka licha ya kuzingatia makundi matano ya vyakula lakini pia amewataka kuanzisha bustani ambazo zitawasaidia kupata mbogamboga zitakazotumika katika vyakula vikuuu huku akisisitiza kutumika kwa mafuta katika vyakula ili watoto waweze kupata virutubishi mbalimbali kama vitamin na vinginevyo.
Aidha amesema kuwa kupitia upatikanaji wa chakula mashuleni idara ya elimu sekondari inatekeleza lengo ya kitaifa la masuala ya lishe kwani pasipo kuwa na afya njema huwezi ukafanya vizuri hususani kwa upande wa wanafunzi pasipo chakula ni ngumu mwanafunzi kujifunza na kufanya vizuri darasani hivyo amewataka walimu hao kuhakikisha wanakuwa na bustani katika shule zao lakini pia kupanda miti ya matunda.
Akizungumzia upande wa watoto wa rika balehe amesema watoto wanaendelea kukua hivyo ni vizuri vyakula vikapatikana katika makundi ya matano kwani mtoto anatakiwa kujengwa vizuri ili viweze kuwasaidia hata katika via vya uzazi na homoni ili wasipate shida pindi watakapokuwa watu wazima ambapo katika ukuaji wanahitaji nguvu nyingi lakini wanapokula vizuri hata akili zao zinakuwa vizuri.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa