Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ametoa agizo kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwachukulia hatua Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani wa wizara hiyo pamoja na maafisa wote waliohusika katika upotoshaji wa mipaka ya eneo la Mabwegere ambayo kwa namna moja ama nyingine umeigharimu Serikali fedha nyingi ili kutatua mgogoro huo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri huyo wakati akikabidhi taarifa ya uchunguzi iliyofanywa na Jaji wa Mahakama Kuu ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacob Mwambegele kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen Kebwe kuhusiana na mgogoro wa mipaka ya kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani vya Matongolo, Dumila, Mbigiri, Mfulu na Mambwegwa vilivyopo wilayani Kilosa.
Lukuvi amesema kuwa taarifa ya uchunguzi ilibaini chanzo cha mgogoro huo ni kukosekana kwa ushirikishwaji wa vijiji jirani katika kuainisha na kuweka mipaka ya kijiji cha Mabwegere jambo lililosababisha kijiji hicho kuwa na eneo la ukubwa wa hekta 10,234 huku kijiji mama cha Mfulu kikiwa na hekta 1,717 jambo linalodhihirisha kwamba mipaka ya kijiji cha Mabwegere kuingia katika kata tatu za Mbigiri, Kitete na Msowero japokuwa kiutawala kijiji cha Mabwegere kinaratibiwa na kata ya Kitete
Aidha niseme wazi Wizara ya Ardhi haijakifuta kijiji cha Mabwegere bali itaanza kutekeleza mapendekezo yaliyotokana na uchunguzi ya kufuta mipaka ya kijiji hicho ambapo kwa sasa utaanza mchakato wa kuanzaa upya mipaka ya vijiji hivyo kwa njia shirikishi chini ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wilaya ya Kilosa.
Kwa mujibu wa taarifa ya jaji Jacob alipendekeza uboreshwaji wa utendaji kazi, weledi, maadili, umakini na uwezo wa kutunza nyaraka za Idara ya Upimaji na Ramani kwa ajili ya kumbukumbu jambo litakalosaidia kuepukwa kwa migogoro ambayo inaweza kuzuilika.
Lukuvi amesema kuwa kuwa Serikali inaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani hivyo ni jukumu la TAMISEMI kwa kushirikiana na Wilaya ya Kilosa kuhakikisha mipaka inaandaliwa upya kwa ajili ya kuanzishwa kijiji upya.
Na nisisitize kuwa shughuli za kibinadamu kama vile ufugaji na kilimo hazihusiani na masuala ya mipaka, hivyo wilaya licha ya kushughulikia suala la mipaka lazima iandae mpango wa matumizi bora ya ardhi na kupendekeza maeneo ya ufugaji huku busara ikitumika kufanya shughuli hiyo.
Naye Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Kakunda amesema wataalam wanapaswa kuacha nidhamu ya woga bali wazingatie kanuni, sheria na taratibu ili kutekeleza majukumu yao na amemwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI kuunda timu ya uchunguzi kuchunguza mchakato mzima wa uanzishwaji wa kijiji hicho na kila atakayebainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mary Mwanjelwa amesisitiza hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wote waliohusika na kusema kuwa Serikali ya awamu ya tano inawajali wananchi wake na iko tayari kutetea maslahi ya wananchi, hivyo haitasita kufukua makaburi lengo ikiwa ni kubaini wote walioidanganya serikali.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa