Chama cha Ushirika Saccos ya Walimu Wilaya ya Kilosa kimepoteza fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.6 baada ya wanachama na wanufaika wengine kukopa na kushindwa kurejesha kwa wakati kutoka mwaka 2007 hadi 2017 ambapo Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Morogoro amemuagiza Mwenyekiti wa Saccos hiyo kuandaa orodha ya majina ya viongozi na watendaji wake ikiwemo namba za simu na mahali wanakopatikana ambapo walikuwepo kipindi hicho kwa kuzingatia muda aliokaa madarakani na kiasi cha fedha kilichopotea ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza katika kikao cha bodi ya Saccos ya Walimu Kilosa kilichofanyika mwishoni mwa wiki Mrajisi Kenneth Shemdoe amesema kuwa inawezekana viongozi hao na watendaji wake hawakuchukua hizo fedha lakini kwasababu walikuwa hawafuati taratibu, sheria na masharti ya chama basi watawajibika kwa mujibu wa sheria ya ushirika ,kifungu cha 126 na kwamba watalazimika kulipa faini kiasi cha shilingi milioni 5 ama kifungo kisichopungua miaka miwili au vyote viwili kwa pamoja lakini pia baada ya kutumikia adhabu hizo atalazimika kulipa hasara aliyosababisha katika chama ambapo pia kwa kuwa fedha hizo ni za umma na kwamba si za mtu binafsi hivyo yeyote aliyeshiriki kuchukua hizo fedha atazitapika na kwamba yeye kama kiongozi atahakikisha zinarudi kwa namna yeyote ile na hakuna hata shilingi itakayosalia mikononi mwa mtu.
Aidha katka kikao hicho wajumbe wamekubaliana kwa pamoja kuweka mikakati ya kukiimarisha chama ambapo pia chama hicho inapaswa kutekeleza maazimio mbalimbali ikiwemo kuhakikisha chama kinaandaa orodha ya wastaafu wote na kuanza kuwalipa kadri fedha zitakavyopatikana, kuongeza wanachama wapya, kutoa mikopo ya dharura ya muda mfupi ambayo itazalisha faida itakayosaidia kukiendesha chama, kufanya taratibu za kupata leseni, kuandaa makisio au bajeti kwa mapato na matumizi na kupitisha katika mkutano mkuu miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha kuanza, kuhakikisha hesabu za fedha zinafika kwa mkaguzi wa nje ambaye ni mkaguzi wa vyama vya ushirika, kutoa fomu za uchaguzi ambapo uchaguzi unatarajiwa kufanyika kabla ya tarehe 31 April mwaka huu , kuwasilisha rasmi ya hesabu kila mwaka kabla ya tarehe 31 Januari, kuongeza hisa, kufanya mikutano kwa mujibu wa sheria ikiwemo mkutano mkuu wa mwaka na kuhakikisha chama kinaendeshwa kwa mujibu wa sheria za ushirika .
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa