Kufuatia tukio la moto uliojitokeza katika soko la Kilombero katika kata ya Ruaha wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa kikosi kazi kilichoundwa ili kubaini chanzo cha moto pamoja na kufanya tathmini ya athari zilizojitokeza kutokana na moto huo.
Wito huo umetolewa Oktoba 12, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga wakati akizungumza na wananchi katika eneo la soko hilo ambapo amesema hadi sasa chanzo cha moto bado hakijajulikana hivyo kikosi kazi hicho kitakutana na mwananchi mmoja mmoja ili kuweza kupata taarifa mbalimbali zinazohusiana na tukio hilo ili kuchukua hatua stahiki.
Aidha amemshkuru Mh. Rais kwa uwepo wa gari la jeshi la zima moto lililoko kata ya Mikumi ambalo limekuwa msaada mkubwa katika kuzima moto uliojitokeza majira ya saa tatu usiku huku akitoa rai kwa kampuni ya Kilombero sugar kuweka mpango wa kununua gari la zima moto ili kujinusuru katika matukio ya moto ambayo yanaweza kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Kisena Mabuba amewasihi wafanyabiashara wote waliojenga maeneo ya ziada katika vibanda ambayo yamepelekea kuziba kwa barabara kubomoa mara moja maeneo hayo ambayo yamepelekea barabara hizo kutopitika jambo lililopelekea ugumu wa zoezi la kuzima moto kutokana na barabara hizo kuwa finyu.
Aidha amewataka wafanyabiashara ambao vibanda vilivyoathirika kuendelea na biashara zao wakati Halmashauri ikiendelea kufanya taratibu nyinginezo kurejesha miund0mbinu ya vibanda hivyo ambavyo ni mali ya Halmashauri huku akisema kuwa pamoja na taratibu za kurejesha vibanda hivyo zoezi la kutafuta mali zilizoibiwa linaendelea huku akisihi ulinzi kuendelea kuimarishwa pamoja kuchukua tahadhari.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa