Serikali imedhamiria kuondoa adha za sekta ya elimu nchini kwa kuwaletea mradi wa Boost ambao umeanzishwa kwa makusudio ya uboreshaji wa miundombinu kwa madarasa ya awali na msingi kwa kuweka mpango wa shule salama
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mtumbatu Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijenga sekta ya elimu nchini ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati.
Profesa Kabudi amewataka wananchi hao kuupokea na kutekeleza mradi wa Boost kwa kushiriki ipasavyo katika utoaji wa nguvu kazi kwenye ujenzi wa shule mpya ya msingi ambayo kwa kiasi kikubwa itapunguza kero ya wanafunzi kusomea nje.
Prof Kabudi amesema kuwa kata ya Mtumbatu imekua ya kwanza kupelekewa mradi wa Boost ambao upo mahususi kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha elimu ya awali na msingi Tanzania katika Nyanja mbalimbali ikiwemo kuboresha miundombinu ya madarasa na kwamba ili kukamilika inahitaji nguvu kazi za wananchi.
Awali akizungumza Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kilosa Bi Zakia Fandey amesema wananchi wa kata hiyo wanapaswa kujivunia kuwa waanzilishi wa utekelezaji wa mradi huo ambao ukikamilika utaondoa adha ya mrundikano wa wanafunzi katika darasa moja na kwa kuwa mradi huo ni shirikishi wanatakiwa kujumuika kwa pamoja ili kuleta matokeo chanya kwa haraka.
Kwa upande wa mratibu wamradi wa Boost wilayani Kilosa Nelson Kiliba amesema mradi huo umedhamiria uboreshaji wa miundombinu,shule salama,kuwaongezea walimu ujuzi na kwa mwaka huu wa fedha umeanza kutekelezwa na mradi huo kwa awamu ya kwanza unatekelezwa katika Kata ya Mtumbatu kwa kujengwa shule mpya yenye vyumba saba vya madarasa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa