Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh Kangi Lugola ametoa onyo kwa wananchi kuacha tabia ya kutumia migogoro kama njia ya kuendesha maisha na kujipatia kipato kutokana na fedha ambazo wamekuwa wakiwachangisha wananchi kwa kisingizio cha kuwa wasemaji katika kuwasilisha kero za wananchi kwa viongozi wakubwa.
Kangi amesema hayo Machi 15 mwaka huu katika mkutano wa hadhara alipotembelea wilaya ya Kilosa katika kata ya Kimamba na kusema kwamba wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia migogoro hiyo kama njia ya kujinufaisha na kujikimu kimaisha kwa kushawishi wananchi wanyonge kukusanya fedha ikiwa ni gharama za kuwawezesha kusafiri hali wakijua fedha hizo hazitumiki kama ilivyokusudiwa.
Sambamba na hayo amewataka wananchi wote kwa ujumla kuachana na hulka ya malumbano na badala yake inapotokea migogoro watumie njia stahiki ikiwemo mabaraza ya ardhi kutatua kero zao kwani vyombo hivyo vipo kwa ajili yao na kwamba kwa kufanya hivyo kutaepusha migogoro isiyo na tija lakini pia amewataka wananchi wenye nguvu ya kifedha kutambua kuwa si ruksa kwa mwananchi yoyote kutumia nguvu ya kifedha ili kupora haki za watu.
Aidha amelitaka jeshi la polisi kufanya kazi zao kwa weledi ikiwemo kulinda raia na mali zao ikiwemo ardhi badala ya kuwatishia na kuwakamata wananchi wanapodai haki zao, huku akiwataka polisi hao kuhakikisha amani inatawala na kwamba askari yoyote haruhusiwi kushiriki katika kupora haki za watu na kwamba wapo kutekeleza amri zilizoamriwa na mahakama ili kuhakikisha mwananchi anapata haki yake.
Kwa upande wa migogoro ya ardhi inayoendelea husuani mgogoro wa ardhi wa shamba la Mauzi Estate Kangi amewataka wananchi kutambua kuwa suala hilo litasimamiwa na Kamishina wa Ardhi na kwamba kwa sasa liko katika sehemu husika linashughulikiwa hivyo wananchi hao wawe watulivu mpaka hapo maamuzi yatakapotolewa.
Pamoja na hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amewataka wananchi kuacha tabia ya kuibua migogoro ambayo ipo katika hatua za utatuzi au iliyotatuliwa pindi wanapotembelewa na viongozi hususan mawaziri kwani viongozi wa Wilaya w hiyoapo ili kutatua migogoro, wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ameir Mbarak amewataka wananchi kuwa wakweli na kuacha tabia ya kauli za uchochezi baina ya viongozi na viongozi na kwa upande wa chama wako vizuri na wako tayari kushughulikia kero za wananchi kupitia madiwani wao.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa