Wito umetolewa kwa wananchi kuendelea kuchangia katika miradi mbalimbali ya ujenzi inayoendelea katika maeneo yao hususani ujenzi wa maabara katika shule za sekondari kwani miradi hiyo imeonekana kusuasua ambapo kila shule ya sekondari ya kata inapaswa kuwa na maabara tatu kwa masomo ya fizikia, kemia na bailojia ambazo ujenzi wake unajengwa kwa kushirikisha nguvu ya Serikali na wananchi.
Wito huo umetolewa na Msaidizi wa Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Anza-amen Ndosa akiwa ameambatana na timu ya menejimenti ya mkoa sambamba na baadhi ya wataalam wa timu ya menejimenti ya wilaya walipokuwa katika ziara ya siku tatu ya kutembelea miradi mbalimbali ya elimu, kilimo na afya lengo ikiwa ni kuona hatua mbalimbali za miradi hiyo na changamoto zake ili kuboresha miradi hiyo iweze kufanya kazi kikamilifu.
Ndosa amesema kuwa wamebaini kuwa asilimia kubwa ya kusimama kwa miradi hiyo kumetokana na wananchi kuiachia Serikali imalizie miradi hiyo ambapo ameshauri wananchi kuendelea kuchangia miradi hiyo kwani wanafunzi wanaosoma katika shule hizo ni vizazi vyao, hivyo ni vema wakaunga mkono juhudi za Serikali kwa kuharakisha umaliziaji wa maabara hizo ili Serikali ijikite zaidi katika kuzipatia shule hizo vifaa ili wanafunzi waweze kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo na kwa nafasi.
MOJA YA MAABARA KATIKA SHULE YA SEKONDARI DUMILA
Akieleza athari za kutomalizika kwa maabara hizo Ndosa amesema kila shule ya sekondari inapaswa kuwa na maabara tatu kama ulivyo mwongozo kwa ajili ya masomo ya sayansi na kwamba ukosefu wa maabara hizo umechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa masomo ya mkondo wa sayansi kutofanya vizuri katika mitihani yao hivyo kupunguza uwepo wa wataalam wa sayansi ambamo ndani yake wapo madaktari, mainjinia na wataalam wengine watokanao na masomo ya sayansi.
SEHEMU YA VIFAA VYA MAABARA KATIKA MOJA YA SHULE ZA SEKONDARI
Aidha katika miradi ya kilimo hususani skimu ya umwagiliaji iliyopo katika kata ya Mvumi timu hiyo ya mkoa imeshauri Halmashauri kuendelea kutoa elimu endelevu kwa wakulima na wananchi kiujumla juu ya utunzaji wa miundombinu ya umwagiliaji ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
UJENZI WA MAABARA UKIENDELEA KATIKA SHULE YA SEKONDARI MTUMBATU
Kwa upande wa miradi ya afya wameshauri Halmashauri kuanza kuandaa wataalam wa afya kwa ajili ya kituo cha afya cha Magubike ikiwemo mtaalam wa dawa za usingizi kwani katika kituo hicho ujenzi wa jengo la upasuaji unaendelea hivyo ni vema maandalizi yakafanyika mapema sambamba na maandalizi ya vifaa huku akiongeza ufanyike utaratibu wa ukarabati wa chumba cha kupumzikia mara baada ya wajawazito kufanyiwa upasuaji.
TIMU YA MKOA, TIMU YA MENEJIMENTI YA HALMASHAURI NA WATAALAM TOKA SHULE YA SEKONDARI MBUMI KATIKA PICHA YA PAMOJA.
Pamoja na hayo Ndosa na timu yake wamesema Serikali kwa sasa ina masuala mengi ya kutekeleza hususani katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa kati ambapo hakutakuwa na fedha kwa ajili ya ujenzi wa maabara hivyo waheshimiwa madiwani, watendaji wa kata na viongozi wa shule, bodi ya shule kukaana wananchi na wadau mbalimbali ili kujadili namna ya kumalizia maabara hizo ambazo zitawajengea mazingira rafiki wanafunzi ya kujifunzia na ufaulu wa masomo ya sayansi utaongezeka.
Licha ya kupokea ushauri, maelekezo na pongezi kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa katika miradi iliyotembelewa katika kata za Mtumbatu, Mvumi, Dumila, Kimamba, Parakuyo, Mbumi, Mkwatani na kata nyinginezo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amesema kwa pamoja timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Kilosa licha ya ukubwa wa Wilaya ya Kilosa wamepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na timu ya mkoa na kwamba watayafanyia kazi kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri kwani timu hiyo ipo tayari kufanya kazi kwa moyo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa