Wito umetolewa kwa wananchi wilayani Kilosa kuendelea kukienzi kilimo kwani ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu na kwamba kwa kupitia kilimo watu wanapata mahitaji yao mbalimbali ikiwemo chakula na fedha (kipato) kwa ajili ya mahitaji mbali mbali katika ngazi ya kaya.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa kilimo Mh. Omary Mgumba wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo kwa mwaka 2019/2020 ambapo amesema kuwa ni vema jamii ikatambua mchango muhimu wa wakulima, wafugaji na wavuvi na wadau wengine (katika kuchangia uchumi wa Wilaya yetu na Taifa kwa ujumla kwani kila mdau katika sekta ya kilimo anayo fursa ya kukuza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Katika uzinduzi wa msimu wa kilimo ambao mwaka huu unasimamiwa na kauli mbiu “Tumia teknolojia za kilimo bora, hifadhi bora, usindikaji na masoko kuinua kipato”.Mgumba amesema makampuni na sekta binafsi zinawasilisha huduma na shughuli zao kwa umma huku wazalishaji ambao ni wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata fursa ya kujifunza teknolojia mbali mbali za kuboresha uzalishaji, usindikaji na masoko.
Aidha ametoa wito kwa wakulima ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ni vema wakulima wakajituma, wakabadilika, kujibidiisha, kupokea na kutumia mbinu bora za kilimo na teknolojia zinazotolewa na wataalam kutoka katika sekta ya umma na sekta binafsi ili kuzalisha zaidi na hivyo kuvipatia malighafi viwanda vilivyopo na vitakavyoongezeka, hali kadhalika ametoa wito kwa wawekezaji na wadau wote kutumia fursa hiyo kuanzisha viwanda vya usindikaji na uongezaji thamani mazao ya wakulima.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa wakulima kujiunga na kuimarisha vikundi na Vyama vya Ushirika vikiwemo vikundi vya uzalishaji, Vyama vya Ushirika vya Mazao (AMCOS) na Vyama vya Ushirika wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) ambavyo ni mkombozi wa wakulima katika kupata mitaji na elimu ya ujasiriamali ambayo itasaidia kuongeza kipato na kujikomboa kiuchumi.
Pamoja na hayo amesisitiza viongozi wote kushirikiana na Kamati zenu za Amani kwenye ngazi mbalimbali ili kuhakikisha ufumbuzi wa kudumuwa migogoro ya wakulima na wafugaji unapatikana ili kila mmoja ashiriki kikamilifu kwenye uzalishaji kwani inapunguza kasi ya uzalishaji mazao na uchumi wa wananchi lakini pia amepongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa Wilaya katika kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa