Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amewataka wananchi kutambua kuwa ugonjwa wa korona si ugonjwa wa kawaida kwani umekuwa ni ugonjwa hatari kutokana na hali za vifo ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika nchi mbalimbali, hivyo amewataka wananchi wote kuchukua tahadhali dhidi ya ugonjwa wa korona kwa kuzingatia maelekezo mbalimbali yanayotolewa na wataalam wa afya huku shughuli mbalimbali katika maisha zikiendelea ambapo pia amesisitiza kila mmoja kuchukua tahadhari ili kuepuka korona.
Mgoyi ametoa rai hiyo Machi 23 mwaka huu wakati akifungua kikao kilichokuwa kikitoa elimu dhidi ya ugonjwa wa korona ambapo kilishirikisha viongozi wa wilaya, viongozi wa dini, viongozi wa taasisi mbalimbali na wataalam wa afya toka hospitali ya Wilaya ya Kilosa ambapo Mkuu huyo wa Wilaya amesema suala la ugonjwa wa korona ni janga ambalo halipaswi kuhusishwa kwa namna yoyote na masuala ya kisiasa kwani ni suala linalohusisha maisha ya watu, hivyo ni vema kila mmoja kwa nafasi yake akalibeba kwa uzito unaostahiki na kuhakikisha jamii inapona dhidi ya ugonjwa huu.
Sambamba na hayo amesema kuwa kutokana na suala la korona kuhusisha maisha ya watu ni vema kila mmoja akautambua vizuri ugonjwa wa korona na kutoa elimu ya tahadhari katika familia, nyumba za ibada kama vile makanisani na misikitini huku akiendelea kusistiza kuwa suala la taarifa mbalimbali pamoja na matamko dhidi ya korona yatakuwa yakitolewa na viongozi ili kutoleta taharuki katika ya jamii.
Akisisitiza tahadhari dhidi ya korona Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amesema kwa kuwa kuambukizwa kwa virusi vya korona ni mawasiliano ya mtu na mtu kwa kubebaba virusi hivyo jambo kubwa na la msingi ni kila mmoja kujitenga kwa maana ya kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima jambo litakalosaidia kuepusha maambukizi ya gonjwa hili ambapo amesema kinga ni bora kuliko tiba na kwamba gonjwa la korona halina tiba hivyo ni vema kuepuka maeneo ambayo ni hatarishi kwani litasaidia kuwa salama na kuepuka maambukizi.
Akitoa elimu dhidi ya ugonjwa wa korona Kaimu Mganga Mkuu Wilaya Dkt. George Kasibante amesema virusi vya korona vinatoka katika familia ya virusi vinavyoshambulia binadamu kupitia njia ya hewa kama mafua ya kawaida ambapo vinaenezwa kwa njia ya majimaji yatokayo katika njia ya hewa ikiwemo SARS na uambukizo mkali wa mapafu na kwamba ugonjwa huo hushambulia mapafu na kufanya upanukaji na ubadilishanaji wa hewa kuwa mgumu na kusababisha mgonjwa kushindwa kupumua.
Kasibante amesema nchini Tanzania korona ilithibitika rasmi 16 Machi, 2020 ambapo mgonjwa wa kwanza alibainika jijini Arusha na baadae Zanzibar na Dar es Salaam hadi sasa kuna wagonjwa 12 ambapo 8 ni watanzania 4 wageni na idadi kubwa ya washukiwa ambao wana historia ya kusafiri katika nchi zinazoshukiwa au kugusana na washukiwa ambapo amebainisha kuwa hadi sasa hakuna taarifa ya kifo chochote kilichoripotiwa hapa nchini huku katika Mkoa wa Morogoro na Wilaya nzima ya Kilosa hakuna kisa chochote cha mgonjwa aliyethibitika kuwa na ugonjwa huo..
.
Akibainisha dalili za haraka za ugonjwa huo amesema ni Homa, kikohozi kibichi, kuhema kwa tabu, maumivu ya mwili, kuuma kwa koo mfano matonses, kukosa hamu ya kula huku dalili za mara chache zikiwa ni kuhara, kutapika, kichwa kuuma, kukohoa damu na maumivu ya kifua ambapo makundi ya watu walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu wakiwa ni wazee zaidi ya miaka 60, watoto chini ya miaka 5, wagonjwa walio na magonjwa sugu na wale waliolazwa hospitalini na majumbani
Akielezea namna ya kujikinga na korona amesema ni kwa njia ya kuosha mikono vizuri kwa maji safi na sabuni, kutumia vikinga pua na mdomo (masks)na uso, kuzingatia walau umbali wa futi 6 kutoka kwa mgonjwa mwenye korona, Hakuna chanjo mpaka sasa ambapo amesema kirusi cha korona katika mwili wa binadamu huchukua siku 2 mpaka 14(wastani siku 5) kwa binadamu kuanza kuonesha dalili baada ya kuambukizwa na virusi vya koron pia huambukizwa kwa njia ya matone yatokanayo kwa kukohoa au kugusana moja kwa moj lakini pia kuepuka kusalimiana kwa mikono
Kwa kutambua uzito wa gonjwa hili Dkt. Kasibante amesema Halmashauri imejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo kuunda Timu ya Dharura ya Halmashauri pamoja na vituo vya afya ambayo imesaidia katika kuelimisha jamii namna ya kijikinga, kutenga maeneo ya kutibu wagonjwa pamoja na kuwashikilia wagonjwa kwa muda wakati sampuli zinapelekwa maabara ya taifa kwa uchunguzi zaidi, kutekeleza uratibu wa karibu katika maeneo yenye watu wengi na mwingiliano wa watu ikiwa ni pamoja na Kambi ya Waturuki, Dumila, Kilosa Kati, Mikumi na Ruaha, kutekeleza utengaji wa chumba maalumu cha kushikilia wahisiwa katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika mamlaka husika kwa hatua zaidi, kutekeleza tathmini ya mahitaji ya awali ya Wilaya na kuwasilisha MSD kwa haraka, kuteua Zahanati ya Kondoa kama kituo kwa ajili ya kutenga wagonjwa waliothibitika kuwa na Virusi vya korona, kupanga uratibu wa utoaji elimu katika ngazi ya jamii, Taasisi na katika Vituo vya kutolea huduma, Kupata taarifa ya kila siku ya wageni hasa kwa waturuki ili kujua ni wageni wangapi wameingia na hali zao za kiafya na kutekeleza tathmini ya kila siku jioni juu ya utekelezaji wa mikakati wa siku husika na kujipanga kwa siku inayofuata.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa