Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa Wananchi Wilayani Kilosa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi huo ili kuwachagua Viongozi Bora watakaowaongoza katika Vijiji na Vitongoji vyao.
Rai hiyo imetolewa 26 Septemba 2024 na Msimamizi wa Uchaguzi Ndg. Michael .J. Gwimile wakati wa kikao cha Maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ambapo amesema ni haki ya Msingi kwa kila mwananchi mwenye sifa kupiga kura na kumchagua kiongozi anayemtaka lakini pia kuchukua fomu ya kugombea nafasi za uongozi ili aweze kuchaguliwa.
Gwimile ameongeza kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa uwazi, haki na usawa utakaozingatia sheria na taratibu zilizowekwa ambapo uchaguzi huo utalenga kuwachagua Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji katika Mamlaka ya Wilaya.
Akizungumza katika kikao hicho, Gwimile amesema zoezi la uandikishaji wa wapiga Kura utaanza kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024 ambapo uandikishaji huo utafanyika kwenye vituo vilivyopo kwenye vijiji na vitongoji husika sambasamba na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika taraehe 27 Novemba,2024.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya Samwel. L. Kijanga ametoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Viongozi wa Dini kuwaelimisha wananchi kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa wakati wa zoezi la Uchaguzi ili kuepuka vitendo vya uvunjifu wa Amani katika maeneo yao, Pia amesisitiza wananchi kutoa Taarifa endapo kutakuwa na viashiria vya uvunjifu wa Amani ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Naye Kamanda wa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya Gwakisa Mwaikela amewataka Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini pamoja na Wananchi kuzifahamu kanuni au makatazo katika kipindi hiki cha uchaguzi kama vile kupokea au kutoa pesa, zawadi, au ahadi mbalimbali ili aweze kuchaguliwa au kujiondoa kuwa mgombea katika uchaguzi au kushawishiwa kupiga kura zaidi ya mara moja ambavyo ni makatazo kwa mujibu wa sheria.
Kikao hicho cha Maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kimeudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Kamati ya Ulinzi na Usalama, pamoja na Wataalam wa Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa