Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja tabia ya kuvamia maeneo yaliyotaifishwa na kubatilishwa miliki mpaka hapo taratibu zote zitakapokamilika ikiwemo kufuatwa hatua stahiki kama kupitishwa kwa mapendekezo husika katika baraza la mawaziri kwa ajili ya kupitishwa kwa mujibu wa taratibu kisha maeneo hayo kugawiwa kwa mujibu wa taratibu za ugawaji ardhi zitakavyokuwa zimependekezwa.
KATIBU TAWALA WILAYA YOHANA KASITILA NA MWENYEKITI WA HALMASHAURI MH. HASSAN MKOPI NI MIONGONI MWA WAJUMBE WA KAMATI YA USHAURI
Mgoyi ametoa rai hiyo Disemba 12 wakati wa kikao cha kamati ya Ushauri Wilaya na kusema kuwa kumekuwa na baadhi ya wananchi wameamua kujimilikisha maeneo katika shamba la mwekezaji Farm Africa na kujigawia baadhi ya maeneo jambo ambalo ni kosa kisheria kwani shamba hili bado halijataifishwa kisheria, hivyo ni vema wananchi wakawa na subira hadi hapo hatua stahiki zitakapokamilika.
Pamoja na hayo ametoa onyo kwa wafugaji wanaokodisha maeneo ya ufugaji kwa wakulima jambo ambalo linaleta migogoro pindi mazao ya wakulima hao yanapostawi vizuri wafugaji hao hupitisha mifugo yao katika mashamba na kusababisha mifugo kula mazao katika mashamba na kusababisha hasara kwa wakulima na kuzua migogoro inayoleta athari ikiwemo mapigano na nyakati nyingine kusababisha vifo.
MKURUGENZI MTENDAJI WA HALAMSHAURI YA WILAYA ASAJILE MWAMBAMBALE
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wajumbe waliohudhuria kikao hicho kuwa Halmashauri kila mwezi hutenga 10% ya mapato yake kwa ajili ya kukopesha vikundi mbalimbali vyenye sifa vya vijana 4%, wanawake 4% na wenye ulemavu 2% lengo ikiwa ni kuwasaidia kujikwamua kwa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo umma utambue kuwa pesa hizo zipo na wasisite kukopa kwani zipo kwa ajili yao.
Akitoa taarifa ya usuluhishi mgogoro wa mpaka wa kijiji cha Ngaite katika kata ya Parakuyo na kijiji cha Kwalukwambe, Malangali, Tindiga A na B kata ya Tindiga kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa idara ya Ardhi na Maliasili Cheyo Nkelege amesema kuwa kutokana na mgogoro huo uliodumi kwamda mrefu yalifanyika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya pamoja ambapo azimio lililofikiwa ni mpaka wa vijiji hivyo ni shamba la mifugo la NARCO uainishwe na kubaini mpaka wake ambapo kazi imeanza na kwamba bado inaendelea kwani kumebaki alama za mipaka nne ambazo hazijaonyeshwa ili kukamilisha zoezi hilo la uhakiki na ubainishaji mipaka.
Aidha kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya kijiji cha Chaumbele A – kilichopo wilayani Kilosa na Kilama kilichopo wilayani Gairo kamati ya Ushauri Wilaya imeridhia kufanyika kwa uhakiki wa majina ya vijiji na vitongoji vyenye mgogoro, kuhakiki na kubainisha mipaka ya vijiji na mipaka ya wilaya za Gairo na Kilosa, kuepuka na kukemea ushawishi wa kisisasa unaopelekea kuwagawa wananchi kwa manufaa ya wanasiasa wachache na kuhakiki upya uanzishwaji wa vitongoji vya Mahedu kilichosajiliwa cha Kilama kilichopo Gairo na vitongoji vya Kikwajuni na Mbuyuni vilivyosajiliwa katika kijiji cha Chaumbele kilichopo Kilosa ili kuwe na vitongoji vyenye hadhi ya kuwa vitongoji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa