Kufuatia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzitaka halmashauri kuweka jitihada za kufufua zao la mkonge kwa kuanzisha vitalu vya kuzalishia miche ya mkonge ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa miche ya mkonge Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa wito kwa wakulima na wananchi kiujumla kujihusisha na kilimo cha zao la mkonge kwani zao hilo lina faida mbalimbali na kuweza kuinua kipato cha mwananchi na wilaya kiujumla.
Akitoa wito huo Februari 2 mwaka huu Mgoyi amewaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali walioshiriki katika kikao cha wadau wa kilimo cha mkonge kuhakikisha wanatenga maeneo katika vijiji vyao ili wananchi walime mkonge kwani wilaya ina ardhi zaidi ya ekari laki mbili inayoweza kulimwa mkonge hivyo maeneo ya kulima mkonge yaainishwe ili kupata maeneo ya kutosha ili kulima mkonge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa Asajile Mwambambale ametoa rai kwa wakulima na wadau mbalimbali kujikita katika kilimo cha mkonge kwani kina faida mbalimbali ikiwemo uwezo wa zao hilo kuvumilia ukame lakini pia lina uwezo wa kuchanganywa na mazao mengine ya msimu kama vile kunde, mahindi, maharage, alizeti, njegere na karanga.
Faida nyingine kuwa mkonge unaweza kupandwa na kuvunwa msimu wowote wa mwaka na mmea wake huishi kwa muda mrefu yaani miaka 10 hadi 25 na huweza kuvunwa kila baada ya miezi 6 hadi 9 kila mwaka hivyo kumhakikishia mkulima kipato lakini pia unastahimili magonjwa, magugu na wadudu na hata upungufu wa rutuba kwenye udongo.
Akibainisha umuhimu na fursa za kulima za zao la mkonge ni wa uwepo kwa mnunuzi wa ndani ambaye ni CHINA STATE FARM, upatikanaji wa mbegu za mkonge (Maotea, na vikonyo) lakini pia Wilaya ya Kilosa kuna eneo linalofaa kwa kilimo cha mkonge hekta 6468 ambalo wakulima wanaweza kulitumia kulima mkonge kwa tija, uwepo wa viwanda vikubwa 3 vya kuchakata mkonge, kuzalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na mkonge hapa nchini pamoja na kukuza pato la Wilaya na Taifa kwa kuuza bidhaa za mkonge kwa mataifa mengine, kuinua uwezo wa viwanda vya ndani kujitegemea na kutoa ajira za kutosha kwa wananchi wa madaraja yote.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa