Kwa kutambua umuhimu na chachu yenye ushawishi katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kamati ya Siasa Wilaya ikiwa imeambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kupitia mradi wa mkaa endelevu imejionea utekelezaji wa utunzaji wa misitu na uvunaji wa mkaa kwenye moja ya vijiji ishirini vinavyoshiriki katika mradi huo katika kijiji cha Chabima kilichopo katika kata ya Masanze.
Akizungumza Februari 3 mwaka huu mbele ya kamati ya hizo Meneja wa Mradi wa Kuleta Mageuzi Katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) Charles Leonard amesema kuwa uanzishwaji wa misitu ya ardhi za vijiji umeweza kusaidia uvunaji endelevu wa rasilimali ambapo mradi huo kwa awamu ya tatu ambao unafanywa na Shirika la kuhifadhi Misitu ya Asili (TFCG) chini ya mradi wa mkaa endelevu unaofadhiliwa na Shirika la Uswisi (SDC) ulianza Disemba 2021 na unatarajiwa kuisha Novemba, 2022 ukiwa na tija ya kuwanufaisha wanakijiji na kuweka mfumo utakaochangiwa na vijiji kwa asilimia saba ambazo zitatumika kutoa mafunzo kwa wanakijiji, kuwasaidia soko na kuhimiza uwekezaji kwenye maeneo yao ambapo amesema vijiji vyenye misitu ya vijiji inatambuliwa kimataifa na imesajiliwa katika kanzi data ya kidunia ambayo itafaidika kwa kuwezeshwa uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi sambamba na maendeleo ya wananchi.
Wakizungumza baadhi ya wanakijiji ambao wamenufaika na Mradi huo Beritha Magaga na Hamis Kimota wamesema kabla ya mradi walikuwa wakijishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji ila baada ya kupatiwa mafunzo na Mradi wa Mkaa Endelevu walihamasika kujiunga kwenye chama cha uvunaji mkaa ambapo kupitia kipato kitokanancho na mkaa wamefanikiwa katika mambo mbalimbali ikiwamo kujenga nyumba, kujikimu katika mahitaji ya kifamilia, kuanzisha biashara ndogondogo na kujiunga katika vyama vya kuweka na kukopa.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya Shaban Shemdoe ameushukuru uongozi mzima unaoendesha mradi huo kwa elimu waliyowapatia na kujionea shughuli za utunzaji wa misitu na uvunaji mkaa unavyofanyika na kuwapongeza wanakijiji wa Chabima kwa utunzaji wa Misitu ya asili ambapo pia amewaomba TFCG kushirikiana na wananchi kuongeza upandaji wa miti ili kufidia iliyovunwa na huku akiwasisitiza madiwani kuendelea kutoa elimu ya utunzaji misitu kwa wananchi ambayo itawasaidia kuwa wasimamizi wazuri katika maeneo yao.
Aidha ametoa rai kwa watendaji wa vijiji kufanya kazi kwa ukaribu na wenyeviti wa vijiji hususani katika shughuli za maendeleo zinazofanyika katika maeneo yao ikiwemo kuwaunga mkono katika miradi wanayoanzisha kwa manufaa ya wananchi
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa