Wananchi wametakiwa kujenga utamaduni wa kusafisha mazingira yao mara kwa mara ili kuepuka madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Wapa Mpwehwe katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Usafishaji Duniani ambayo Kiwailaya imeadhimishwa kwa kufanya usafi katika soko la Sabasaba.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Ndg. Mpwehwe amewataka wakazi wa kilosa kusafisha mara kwa mara mazingira yao ya nyumbani pamoja na maeneo wanapofanyia shughuli zao huku akiwataka wananchi kufanya usafi wa pamoja kila siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo Kilosa Grace Chogongwe na Mwenyekiti wa mamlaka hiyo Hussein Fadhili wameutaka uongozi wa soko hilo kuweka utaratibu wa kusafisha soko hilo mara kwa mara.
Naye Mhe Diwani wa kata ya Kasiki Mhe. Ramadhani Mpangachuma na Diwani wa kata Mbumi Mhe. Shabani Maringo Wameushukuru Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa Kuratibu zoezi hilo la usafi ndani ya soko la Sabasaba.
Siku ya usafishaji Duniani huadhimishwa kila ifikapo 20 Septemba kila mwaka huku maadhimisho ya mwaka huu yakiwa yamebebwa na kaulimbiu isemayo: “Uhai hauna Mbadala, tuzingatie usafi wa mazingira”
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa