Wananchi Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wametakiwa kutunza Miundombinu ya Barabara inayojengwa na Serikali ikiwa ni pamoja na vyuma vya madaraja ili kuwezesha Miundombinu hiyo kudumu muda mrefu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Kauli hiyo imetolewa machi 10, 2024 na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dokta Mussa Ally Mussa wakati wa Ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ya kutembelea Miradi ya Maendeleo ya Sekta ya Miundombinu hususan barabara zinazojengwa Wilayani hapa.
Dokta Mussa Ally Mussa ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Kighoma Malima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa,amesema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwaajili ya maendeleo lakini kuna watu wachache wanarudisha nyuma juhudi na azma ya Serikali ya kuwaletea Wananchi wake maendeleo jambo ambalo siyo jema,amewasisitiza wanachi wote kwa umoja wao kulinda na kuitunza miundombinu hiyo.
Aidha amewataka Wananchi wanaoshi Berega na vijiji vya jirani na Daraja hilo linalounganisha Mkoa wa Morogoro na Tanga kuungana na kupanda Miti pembezoni mwa mto huo kwaajili ya kuimarisha daraja hilo hususan Mikarafuu kwani mbali ya kuimarisha daraja lakini pia itawapatia faida kubwa kiuchumi.
Katika Ziara hiyo Wilayani Kilosa Wajumbe hao wa Kamati ya Ulinzi na usalama Mkoa ikiongozwa na Katibu Tawala wametembelea Daraja la Mto Berega, Daraja la Mto Mzinyungu, Daraja la mto Ilonga, Barabara ya Rudewa – Kilosa, Daraja la mto Ruaha Mkuu, Daraja la Ruhembe,na Barabara ya Mikumi Ifakara.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa