Wananchi Wilayani Kilosa wametakiwa kujitokeza kushiriki zoezi la uandikishaji au uboreshaji wa taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi mkuu na kumchagua kiongozi wamtakaye ifikapo Oktoba , 2025.
Wito huo umetolewa Machi 1, 2025 na Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka wakati akitembelea vituo mbalimbali vya uandikishaji vilivyopo katika jimbo la kilosa na mikumi ambapo Mhe. Shaka amesema ili mwananchi aweze kumchagua kiongozi anayemtaka kama vile diwani, Mbunge na Rais ni lazima ajiandikishe au kuboresha taarifa zake katika zoezi hilo.
Aidha, Mhe. Shaka amewasihi makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo makundi ya vijana, viongozi wa dini na taasisi zisizo za kiserikali kuendelea kuhamasishana kujitokeza kushiriki zoezi hilo umuhimu ambalo litaendelea hadi kufikia Machi 7, 2025.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bi. Beatrice C. Mwinuka amesema zoezi hilo ni rahisi na halichukui muda mrefu hivyo amewataka wananchi kujitokea kujiandikisha au kuboresha taarifa zao ili waweze kupata haki ya msingi ya kikatiba.
Naye Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kilosa na Mikumi Ndg. Betuely Ruhega amesema zoezi hilo litahusisha makundi mbalimbali ikiwemo kundi la waliofikisha miaka 18, waliopoteza au kuharibika kwa vitambulisho vyao pamoja na wale waliohamia kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa