Wananchi Wilayani Kilosa wametakiwa kutambua maana,visababishi, madhara na namna ya kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia ili kuweza kuupunguza au kuutokomeza kabisa kuanzia ngazi ya familia, kijamii na kadhalika.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Hakiardhi Bw Cathbert Tomitho Novemba 19,2024 Wakati wa Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto iliyofanyika katika kijiji cha Kitange ii, Kata ya Mtumbatu Wilayani humo ambapo amesema kuwa Mila na desturi katika maeneo mengi Nchini hazimpi nafasi na uhakika mtoto wa kike kumiliki ardhi licha ya kuwa wao ndiyo walimaji na watunza familia.
Amebainisha kuwa hali hiyo inatokana na malezi na mfumo dume ambao umekuwepo kwenye Jamii kwa miaka mingi,hivyo muda umefika wa jamii kubadilisha Mtazamo na ndiyo maana elimu juu ya ukatili wa kijinsia inatolewa ili kila mmoja kwa nafasi yake aweze kutambua na kuelewa maana, Visababishi, na mdhara yatokanayo na ukatili huo.
Amesema kuwa lazima jamii ikemee kila aina ya Ukatili, kwa namna yeyote ile ili kujenga jamii iliyo bora hivyo anaamini kupitia mijadala mbalimbali Wananchi wataelewa na kuweza kukabiliana na suala hilo kwani Mijadala inatoa fursa ya kila mmoja kuzungumza na kuweka maazimio ya pamoja juu ya kuondokana na Unyanyasaji katika jamii.
Amewaasa Wananchi wasiache wala kuchoka kuripoti katika sehemu husika pindi wanapofanyiwa ukatili,au kuona mtu anafanyiwa ukatili huku akitaja baadhi ya matukio ya kikatili yaliyokithiri kwenye jamii ikiwemo ubakaji,ulawiti,kunyimwa haki ya kusoma,kupigwa na kadhalika.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Bertila Pascal Ruyumbiza Amewasisitiza Wananchi kuripoti kwenye Madawati ya Kijinsia, kwa watu wanao waamini ikiwemo Walimu, au kupiga simu bure katika namba maalum 116 iliyotolewa na Serikali ili waweze kusikilizwa pindi wanapoona wamefanyiwa ukatili wa aina yeyote ili kuhakikisha kuwa Yule anayefanya vitendo hivyo anawajibika kwa matendo yake na kuwa fundisho kwa wengine.
Aidha amewataka Wazazi kuacha tabia ya kuwalaza watoto chumba kimoja na jamaa au ndugu au wageni wanaokuja kuwatembelea kwani ripoti nyingi zimebainisha kuwa matukio mengi ya ubakaji yanafanywa na watu wa karibu.
Kampeni hiyo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto Wilayani Kilosa imefanyika kwa ushirikiano kati ya Divisheni ya Maendeleo ya jamii na Taasisi ya Hakiardhi dhima ikiwa ni CHAGUA kutokomeza Ukatili wa Kijinsia.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa