Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi kupitia kampeni FURAHA YANGU - PIMA, JITAMBUE, ISHI MWANAUME JALI AFYA YAKO, PIMA VVU amehawamasisha wanaume kupima ili kutambua hali zao za maambukizo ya VVU na kuanza ARV mapema kwa wale watakaogundulika kuwa na VVU kwani wanaume wengi wana tabia ya kumsindikiza mama apime, na akionekana yupo salama mwanaume anajiweka kwenye kundi salama jambo ambalo sio sahihi.
Mgoyi amesema kuwa kupitia Kauli mbiu ya FURAHA YANGU – PIMA, JITAMBUE, ISHI tunatupata mwongozo wa kampeni kwa kutufahamisha umuhimu wa kupima VVU, ili kujitambua na kuishi kwa furaha kwani wale wanaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU wanapaswa kuanza dawa za kufubaza VVU (ARV) mapema na kuishi kwa furaha wakitekeleza majukumu yao binafsi, ya kifamilia na ya Kitaifa .
Aidha amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuanzisha kampeni hii ya kuhamasisha wananchi kupima VVU, hususan wanaume, na kuanza ARV mapema mara wanapogundulika kuwa na maambukizi kama ilivyoelezwa na Waziri wa Afya, tangu Oktoba 2016, Serikali iliridhia mpango wa kupima VVU na kuanza dawa mara moja, yaani “TEST and TREAT”, bila kujali kiwango cha upungufu wa kinga ya mwili (yaani CD4). Hivyo, mpango huu una lengo la kumwanzishia dawa za ARV kila mtu aliye na maambukizo ya VVU ili aweze kuishi maisha ya FURAHA bila kuwa na hofu ya kupata magonjwa nyemelezi.
Pamoja na hayo matokeo ya awali ya Utafiti wa Nne wa viashiria vya VVU/UKIMWI (Tanzania HIV Impact Survey – THIS), uliozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani mwaka Jana (Desemba Mosi, 2017) yanaonesha pamoja na mambo mengine kuwa hamasa miongoni mwa wananchi na hasa wanaume katika kuziendea huduma za upimaji wa VVU nchini ni ya kiwango cha chini, hivyowito kwa watu wote, husus nitoe kwenu hasa wanaume kujitokeza kwa wingi kupima VVU kwani wataalamu wapo sio tu kupima VVU bali hata magonjwa mengine sugu kama vile uchunguzi wa awali wa Tezi Dume, Shinikizo la Damu na Uchunguzi wa Lishe
Mimi binafsi nimeamua kuwa KINARA (CHAMPION) wa kuhamasisha wanaume kupima na kuanza dawa mapema kwa wale wanaogundulika na maambukizo ya VVU. Natumia fursa hii kuujulisha umma wa jamii ya Kilosa kuwa nimeridhia kuwa KINARA WA KUHAMASISHA wanaume Wilayani Kilosa wajitokeze kwa wingi kutumia huduma hizi na ninawahamasisha viongozi wenzangu, hususan wanaume, katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini kutumia kauli mbiu hii kwenye majukwaa yao kuhamasisha wanaume kushiriki kikamilifu katika upimaji wa VVU na kuanza dawa mapema kwa wale wanaokutwa na maambukizi.
Aidha Mgoyi ameagiza wataalamu wa afya kupanua afua za kitabibu za uthibiti wa VVU na UKIMWI pamoja na kupanua wigo wa kuwatumia wanaogundulika na maambukizi ya VVU kuwaleta wenza wao sehemu za kupata huduma, kuimarisha fursa ya wahudumu wa afya kwa magonjwa mengine, kuwashawishi watumiaji wa huduma hizo kupimwa, kuwatumia wasanii ili kuhamasiha mabadiliko ya tabia hasa katika kupima virusi vya ukimwi mapema, kupanua huduma za upimaji na ushauri nasaha katika vituo vya kutolea huduma za afya na hata katika maeneo yenye mikusanyiko.
Pia kuainisha na kutumia maeneo ya shughuli za kiuchumi, kijamii, kidini, kimila na starehe yanayowaleta wanaume pamoja ili kuwahamasisha wanaume kuziendea huduma za upimaji wa VVU na magonjwa mengine sugu kwani utaratibu huo utaleta matokeo chanya hasa kwa kuwatumia wanaume ambao ni viongozi na wanaheshimika katika maeneo husika, kuziunganisha huduma za upimaji wa VVU katika upimaji na huduma za magonjwa mengine kama magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ili kuimarisha upatikanaji wa huduma katika sehemu moja kwani jambo hili litawavutia wengi, hasa wanaume katika kupata huduma za upimaji wa VVU wakati wakipata huduma nyingine zenye manufaa kwa afya zao, Pia viongozi wa dini katika nyumba za ibada, wahamasishe wananchi haswa wanaume kujitokeza kwa wingi na kupima VVU na endapo wakigundulika basi waanze dawa mara moja
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa