Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Wilaya ya Kilosa imefanya maadhimisho ya kiwilaya Machi 5, 2025 katika Kijiji cha Mbwade kilichopo Kata ya Madoto ambapo Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, ambapo amewapongeza Wanawake kwa jitihada zao za maendeleo na kuwataka kutumia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema "Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki,Usawa na Uwezeshaji" kama njia ya kujikwamua kiuchumi na kushiriki kwa haki katika uongozi wa nchi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe Shaka Hamdu Shaka ametoa pongezi kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa hatua mbalimbali alizochukua katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa nyingi za maendeleo na kwamba, fursa hizo zinapaswa kutumika kwa namna bora na kwa uzalendo, ili wanawake waweze kujenga jamii imara na kuleta maendeleo katika sekta zote za maisha
Aidha katika hotuba yake, Mhe. Shaka Mhe. Shaka amewashauri wanawake na wasichana wa Wilaya ya Kilosa kutambua nguvu waliyonayo na kuitumia vizuri kwa manufaa yao na ya jamii ambapo amesema Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwaletea miradi na fursa za maendeleo, lakini pia ni jukumu lao kama Wanawake kutumia fursa hizo kwa ustawi wa familia zao na kwa maendeleo ya jamii.
"Rais Samia amefanya kazi kubwa kwa kuwapatia wanawake fursa za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na mikopo ya Halmashauri na miradi ya maji na hizi ni hatua kubwa ambazo zimewakomboa wanawake na kuwawezesha kujitegemea," alisema Mhe Shaka.
Aidha Mhe. Shaka ametoa wito kwa wanawake na wasichana wa Wilaya ya Kilosa kutumia fursa zinazotolewa na serikali na ili kuwa na maisha bora na kuleta mabadiliko ya kweli huku akiwataka kushiriki katika kugombea nafasi za mbalimbali za Uongozi, kushirikiana katika shughuli za kiuchumi, na kujitolea kwa jamii zao.
"Wanawake wanapaswa kujitokeza kwenye nafasi za uongozi ili kuleta mabadiliko ya kweli na wanaweza kuwa viongozi bora na wangeweza kuchukua nafasi zaidi katika serikali," alisema Mhe. Shaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Ardhi Kilosa, Cuthbert Tomitho, amewakumbusha wanawake kuhusu haki yao ya kumiliki ardhi huku akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wanawake kufahamu haki zao na kuzitumia ili kuleta maendeleo kwenye familia zao.
"Wanawake wanapaswa kujua haki zao za kumiliki ardhi, kwani kumiliki ardhi ni haki ya msingi ya kila mmoja, na wanawake wanapaswa kutumia haki hii kujenga familia zao na kusaidia katika shughuli za kiuchumi," alisema Tomitho.
Naye Wakili wa Taasisi ya Haki Ardhi Kilosa, Charles Ndaki, ameongeza na kusema kuwa haki ya kumiliki ardhi ni sawa kwa wanawake na wanaume, na hakuna kizuizi cha kisheria kinachowazuia wanawake kumiliki ardhi.
"Wanawake wanastahili kuwa na haki sawa na wanaume kumiliki ardhi. Hii ni haki ya kikatiba na sheria zote za ardhi zinawawezesha kumiliki ardhi bila vikwazo yoyote," alisema Ndaki.
Kwa upande wao Wananchi wa Kijiji cha Mbwade wameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa kufanikisha sherehe hizo za Siku ya Wanawake Duniani, na kusema kuwa wamefurahi kuona kwamba wamepata Elimu ya haki zao za msingi, hususan katika kumiliki ardhi na kwamba, elimu hiyo imetoka wakati muafaka na itawasaidia kufahamu na kutafuta haki zao kwa mujibu wa sheria.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa