Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael Gwimile amewataka Wataalamu na Wasimamizi wa Kamati ya huduma ya Mikopo ngazi ya Kata kusimamia vema Utoaji wa Mikopo ya asilimia kumi kupitia mafunzo waliyopewa ili mikopo hiyo iweze kuvikwamua vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kiuchumi.
Gwimile ameyasema hayo 4 Oktoba, 2024 wakati akifungua mafunzo ya Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya 10% katika Ukumbi wa Chuo cha FDC Ilonga akifafanua kuwa Serikali imewaamini na kuwapa dhamana hiyo, hivyo ni wajibu wao kuyazingatia mafunzo waliyopewa ili kuleta mabadiliko na kufanikisha mpango wa serikali wa kusaidia makundi hayo kupitia utendaji wao na usimamizi mzuri.
Aidha, ameongeza kuwa mikopo hiyo ni kwa ajili ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu ambao wanatakiwa wawe wamejiunga kwenye vikundi vilivyoisajiliwa, kuhakikiwa na mamlaka husika pamoja na wanavikundi hao kuwa na shughuli maalumu inayotambulika ya kuwaingizia kipato.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Alto Mbikiye amesema mafunzo hayo yataongeza uelewa wa kusimamia utoaji na urejeshaji wa Mikopo ambapo mwaka huu wanatarajia kutoa mikopo ya sh. Bilioni 1.2 ambazo zimekuwa zikitengwa tangu kusitishwa kwa mikopo hiyo.
Pia Mbikiye ameongeza kuwa wanavikundi watakaoomba na kukidhi vigezo vya Mkopo ndio watakaopewa mkopo huo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa vilevile mafunzo hayo yataendelea kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 04 hadi 06 Oktoba 2024 yakiwahusu Maafisa Maendeleo ya jamii ili kuwajengea uwezo ambapo jukumu lao ni kupokea maombi kutoka kwenye vikundi, kuyapitia na kuhakiki kama yamekidhi vigezo vinavyohitajika.
Naye Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya Gwakisa Mwaikela amewasihi kusimamia vema kwa kufata utaratibu na kuhakikisha vikundi hivyo vinakuwa na wajumbe tofauti tofauti na si ndugu pia vikundi hivyo visiwe na mjumbe ambaye ni kiongozi wa serikali au kupokea fedha kwa lengo kupitisha mikopo kwa kufanya hivyo itaisadia vikundi hivyo kuleta mabadiliko chanya na itarahisisha mambo mabalimbali yatakayopelekea kikundi kukua na kujiinua kiuchumi.
Pamoja na mambo mengine wasimamizi hao wamekula kiapo cha kuepuka mgongano wa masilahi wakati wa utoa wa mikopo hiyo kwa walengwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa