Wasimamizi wasaidizi ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji wametakiwa Kutoa elimu kwa wananchi ili wapate uelewa juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi wa serikali za Mitaa ili waweze kuchagua viongozi bora.
Wito huo umetolewa 30 Septemba, 2024 na Msimamizi wa Uchaguzi Ndg. Michael J Gwimile wakati akifungua mafunzo ya Uchaguzi kwa wasimamizi hao ambapo amesema kuwa ili wananchi waweze kujitokeza kwa wingi ni lazima wapate ufahamu kuhusu umuhimu wa kupiga kura na kugombea nafasi za uongozi katika vijiji na vitongoji vyao.
Gwimile ameongeza kuwa ili uchaguzi uwe bora na kupata viongozi bora, unategemea ubora wa kazi zao na uaminufu wao na endapo viongozi bora watapatikana watasaidia Kilosa kuwa na maendeleo hivyo wana jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wenye sifa wanajitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Pia Gwimile amesema wasimamizi hao wasaidizi wana jukumu la Kusimamia, kuendesha na kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi ikiwa ni pamoja na kudumisha Demokrasia, Amani, Utulivu na Mshikamano sambamba na kutenda haki kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa Mafunzo ya Uchaguzi ambaye pia ni Msimamizi Msaidizi ngazi ya Wilaya Batuely Ruhega amesema ni muhimu kuzingatia Kanuni, Sheria na Miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili uchaguzi huo uwe wa haki na uaminifu kwa wapiga kura na wagombea wa nafasi za uongozi.
Batuely amesisitiza kuwa ili Uchaguzi uweze kwenda vizuri wanatakiwa kusimamia kwa kufuata kanuni za uchaguzi zilizowekwa ambazo zitawasaidia kuwaongoza katika utekelezaji wa Majukumu yao kwa dhamana waliyopewa ili kupata viongozi bora watakao ongoza baada ya uchaguzi huo.
Pamoja na hayo wasimamizi wasaidizi hao walikula kiapo cha uaminifu na kutunza siri.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa