Naibu waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji Machi 1 mwaka huu amewataka watanzania wote kujiunga na vikundi vya mikopo vilivyosajiliwa ili kujiendeleza kiuchumi na kulifanya taifa la Tanzania kuwa na uchumi wa kati na zaidi kuwa na nchi inayoendelea kwa kuwa hakuna atakayeweza kuijenga Tanzania bali ni sisi wenyewe.
Amesema hayo wakati akijibu risala iliyotolewa na wana vikoba wa Mikumi, Kidodi na Ruaha kuwa hadi sasa sheria imeshapitishwa ya kutambua vikoba vyote vilivyosajiliwa na kuahidi kuwalinda mahali popote walipo ili wasidhulumiwe tena.
Aidha Kijaji amewataka viongozi wa Wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji kutekeleza sheria ya huduma ndogo ya fedha kwa vitendo kwa kusajili vikoba vyote na kuvipa mikopo pindi inapohitajika huku akiwataka wanavikoba hao kutumia changamoto walizo nazo kuwa fursa.
Pia amewataka wanavikoba kuwa na malengo pindi wanapochukua mikopo hiyo na kubadilisha maisha kwa kuonyesha mfano mwema ili kuwavuta na wengine kujiunga na vikoba hivyo.
Sambamba na hayo Dkt. Kijaji amechangia fedha taslim kiasi cha shilingi 500,000/= kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa shirikisho la wanavikoba wa kata ya Ruaha.
Nao wanavikoba wa kata zote tatu wamewaomba viongozi kuwatembelea mara kwa mara na kuwapatia mafuzo zaidi ya vikoba ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa juhudi na weledi.
Hii imekuja baada ya Rais John Pombe Magufuli kuwataka wananchi kujiunga na vikundi vya kukopa ili kukuza uchumi na kuhakikisha wanapunguza tozo yaani riba hasa kwa wanawake pindi wanapokopa na kuahidi kuwapa wanufaika hao maeneo ya kujenga viwanda vidogovidogo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa