Watendaji wa Kata wametakiwa kutoa elimu kwa wazazi juu ya muhimu wa lishe bora kwa wanafunzi ili waweze kuchangia chakula hasa wakati wa mavuno na kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata chakula bora mashuleni.
Rai hiyo imetolewa 20 Novemba, 2024 na Katibu Tawala Wilaya Bi. Salome Mkinga wakati akiongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa robo ya kwanza kuanzia julai hadi Septemba 2024 ambapo amewataka watendaji kuelimisha wananchi athari za watoto kukosa lishe bora na kupelekea kushuka kwa ufaulu.
Ameongeza kuwa ili kuendana na Teknolojia ya sasa watoto wanahitaji kuwa na fikra na uwela mzuri hivyo ili kutokomeza udumavu wa fikra na kuijenga Tanzania yenye viongozi makini wazazi na walezi wanapaswa kuwapa lishe bora Watoto.
Bi. Salome ameeleza kuwa ni muhimu viongozi kuanzia ngazi ya wilaya na kata kuwajibika na kusimamia vyema suala la lishe kwa kushirikiana pamoja ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii zao lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula mashuleni.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ndg. Seleman Kasugulu amesisitiza viongozi kuanzia ngazi ya kata kushirikiana na kuiga mifano kwa kata jirani zinazofanya vizuri katika suala la lishe ili kupata uzoefu na kuleta matokeo chanya.
Pia Kasugulu ametoa wito kwa watendaji wa kata kuendelea kusimamia na kufuata sheria ndogo za kijiji zilizopo kwa sasa zinazohusu suala la lishe ili ziweze kuwajibisha wale watakaoenda kinyume ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa