Watendaji wa vijiji na kata wamekumbushwa kufanya majukumu yao kwa kuzingatia sheria taratibu na kanuni ikiwemo utatuzi wa kero za wananchi ambapo pia kuendelea kuunganisha mnyoyoro wa utatuzi wa kero katika maeneo yao kwa kuwafikia wananchi na kusikiliza kero zao na kuzitatua huku wakitakiwa kutolea taarifa kwa viongozi wa juu kero ambao zimeshindwa kutatuliwa badala kusubiri wananchi kubainisha kero hizo wanapotembelewa na viongozi wa juu.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale katika kikao kazi kilichoshirikisha timu ya menejimenti ya halmashauri, maafisa tarafa, watendaji wa kata na vijiji ambapo amesema kuwa watendaji wa vijiji wanapaswa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao ili kuwasikiliza kero zao na kuzitatua huku akitaka kero ambazo ziko nje ya uwezo wa watendaji wa vijiji zifikishwe kwa watendaji wa kata kwa ajili ya utatuzi lakini pia taarifa za kero pamoja na hatua zilizochukuliwa dhidi ya kero hizo ziweke katika maandishi ili kutunza kumbukumbu ambazo pia ziwasilishwe kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.
Aidha amewataka Watendaji wa kata kutengeneza mpango kazi wa kutembelea katika vijiji ili kuwezesha, kutambua changamoto za vijiji kutofanya kazi zake vizuri sambamba na kutoa ushauri kwa Mkurugenzi kuhusiana changamoto mbalimbali zinazojitokeza badala ya kusubiri viongozi wakubwa kuja kutatua changamoto hizo lakini pia amewataka kutambua kuwa wako katika kata kwa niaba ya mkurugenzi huku akiwataka maafisa tarafa kuwa na utaratibu wa kufatilia utendaji kazi wa watendaji endapo wanazingatia taratibu na sheria za nchi ili mlolongo mzima wa utendaji kazi uweze kufanya kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria zinavyotaka.
Kwa upande wa utawala bora Mkurugenzi Mtendaji ametaka kufuatwa kwa vikao vya kisheria katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kijiji na kata kwani ni vikao vya lazima na kwani Serikali inafanya kazi kwa njia ya vikao na kwamba Serikali ya kijiji inafanya kazi kwa vikao hivyo ameelekeza vikao vya kisheria vifanyike inavyopaswa huku akitaka kila kijiji kutoa ratiba yake ya mwaka mzima ya vikao vikuu na vya kisheria na kwamba mtendaji yoyote atakayebainika kutofanya vikao hivyo kwa mujibu wa sheria za umma hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake na kwa yoyote ambaye atakutana na changamoto yoyote ya kutofanyika vikao hivyo atoe taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji.
Sambamba na hayo amewataka watendaji wa kata kuhakikisha wanafanya vikao vya kisheria kwa ngazi ya kata na kwamba vikao hivyo ni lazima kwani Serikali ya awamu ya tano haitamvumilia mtendaji yoyote ambaye atakiuka maelekezo ya Serikali, aidha ametaka ndani ya vikao hivyo kujadiliwa kwa taarifa ya mapato na matumizi lakini pia taarifa hizo za vikao na maamuzi yakeziwasilishwe moja kwa moja kwa Mkurugenzi Mtendaji huku akiwaagiza Maafisa tarafa kusimamia zoezi la makabidhiano ya ofisi kwa vijiji vyote ambavyo havijafanya makabidhiano baina ya uongozi uliopita kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na viongozi waliochaguliwa kwani wapo baadhi ya viongozi waliopita wamebaki na nyaraka mbalimbali za ofisi za serikali za vijiji.
Kwa upande wa ukusanyaji mapato amesema hali ya makusanyo wa mapato sio nzuri hivyo ameekeza watendaji wote kukusanya mapato ya Serikali kutoka katika sekta zote ikiwemo mashamba, minada, mahoteli na maeneo mengine kwa kufanya usimamizi wa makusanyo ili kufikia malengo ambayo Halmashauri iliyojiwekea na kwamba kila mtendaji atapimwa utendaji wake kupitia makusanyo kwani asilimia kubwa ya watendaji kazi ya makusanyo wameitelekeza kwa mawakala kwani vyanzo vipo ila havisimamiwi ambapo pia amewataka watendaji kuhakikisha pesa zote zinazokusanywa kupitia mashine za ukusanyaji POS kupelekwa benki kwa wakati kila zinapokusanywa badala ya kuendelea kukaa nazo kwani ni pesa za Serikali hivyo hawapaswi kuzitumia kwa namna yoyote ile.
Pamoja na hayo Mwambambale ametoa agizo kushughulikiwa kwa mtendaji wa kata ya msowero Hassan Kundumu kwa kosa la kumdhamini mtuhumiwa aliyeshitakiwa na Mkurugenzi kwa kutumia pesa za Serikali ambapo mtuhumiwa alishitakiwa lakini mtumishi huyo alimdhamini hivyo kukwamisha dhamira ya kukusanya pesa ya Serikali huku akitoa onyo kwa watumishi kutoingilia maamuzi ya kiongozi anapofanya maamuzi kwa maslahi ya umma.
Pia amewakumbusha watendaji hao kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa korona hivyo amewataka kuendelea kuelimisha jamii kuchukua tahadhari za maambukizi ya virusi vya korona kwa kutoa elimu namna ya kudhibiti virus hivyo kwani kutodhibiti ugonjwa wa korona madhara yake ni kuyumbishwa kwa uchumi.
Kwa niaba ya maafisa tarafa wenzake Afisa tarafa wa tarafa ya Magole Moses Nchimbi na Spora Mgana ambaye ni mtendaji wa kijiji toka Magomeni wamesema wanamshukuru Mkurugenzi Mtendaji pamoja na timu ya menejimenti kwa kuwakumbusha majukumu yao na kwamba wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa kwao na wako tayari kuyafanyia kazi kila mmoja kwa nafasi yake na kuyatekeleza kwa uaminifu kama sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma zinavyoelekeza huku wakiahidi kutembelea wananchi ili kutatua kero zao kama inavyowapasa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa