Imeelezwa kuwa lengo la Serikali katika sekta ya afya ni kwenda sambamba na mikakati ya kidunia katika kupunguza vifo vya watoto kwa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa chanjo za kutosha kwa magonjwa yote yanayopaswa kupatiwa chanjo pamoja na utoaji wa kinga jambo litakalosaidia kupunguza vifo vya watoto.
Mkuu wa Wilaya Comrade Shaka H. Shaka akikata utepe ishara ya uzinduzi wa chanjo ya Surua na Rubella
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Comrade Shaka Hamdu Shaka wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Surua na Rubella iliyofanyika katika viwanja vya kliniki ambapo amesema katika kuunga mkono juhudi za Serikali, Wilaya ya Kilosa imekusudia kuwafikia watoto 74,508 wanao kuanzia umri wa miezi 9 hadi 59 ili kuhakikisha wanapata chanjo ya Surua na Rubella ambapo kampeni hiyo ni kuanzia Februari 15 hadi 18, 2024.
Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji na Mganga Mkuu wakiteta jambo
Katibu Tawala Wilaya Salome Dismas
Shaka amesema Serikali katika kunusuru maisha ya watoto kipaumbele kimewekwa kwa watoto kwa kuwawekea mazingira mazuri ya ukuaji wao ikiwemo upatikanaji wa chanjo huku akiwahamasisha wananchi waliohudhuria tukio hilo kuwa wahamasishaji wazuri kwa wenzao kupitia kaulimbiu ya mpende mwanao mpeleke akapate chanjo.
Mkurugenzi Mtendaji Michael Gwimile akiwa na Mganga Mkuu Wilaya Dkt. Mameritha Basike
Kwa upande wake Mganga Mkuu Wilaya Dkt. Mameritha Basike amesema walengwa wa chanjo ya Surua na Rubella ni watoto chini miaka mitano na kwamba lengo la chanjo hiyo ni kuzuia watoto kupata ugonjwa wa surua ambao hauna tiba na madhara ya ugonjwa huo ni homa ya mapafu, upofu, na vifo huku akitoa rai kwa viongozi wa chama na dini kushiriki katika kuhamasisha jamii ili watoto lengwa waweze kupata chanjo.
Nao wazazi waliowaleta watoto kupata chanjo ya Surua na Rubella wameishukuru Serikali na uongozi wa Wilaya kiujumla kwa kuwafikishia chanjo hiyo kwani wanaamini chanjo hiyo itawasaidia watoto kutopata ugonjwa wa Surua na Rubella na kwamba wanaamini afya za watoto wao zitakuwa vizuri.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa