Watu watatu wamefariki dunia huku kaya zaidi ya 300 zikiarithika baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko Wilayani Kilosa ambapo kata ya Rudewa na Mvumi zimeonekana kuathirika kwa kiasi kubwa.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya Mhe. Shaka Hamdu Shaka Disemba 06,2023 amewataja marehemu hao kuwa ni Iddi Abdalah mwenye umri wa miaka 63 na kwamba kifo chake kimetokea baada yeye na mkewe kujaribu kuvuka mto, ndipo maji yalipomzidia na kumsomba,pia vijana wengine wawili wa kiume ambao miili yao imepatikana siku ya pili baada ya tukio hivyo kufanya idadi ya vifo hivyo kuongezeka.
Mhe Shaka amefafanua kuwa mafuriko hayo yaliyoathiri takribani Kaya Zaidi ya 300 na kuacha mwananchi 400 bila makazi baada ya nyumba 35 kuanguka, yamesababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mikoa ya Dodoma, Manyara na Singida hivyo kupelekea kingo za Mto Wami kubomoka na kuacha njia kisha kusababisha mafuriko hayo.
Mhe. Shaka amesema kutokana na kadhia hiyo Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wamefanya jitihada za awali ikiwa ni Pamoja na kutenga maeneo ya shule kwa ajili ya kuwahifadhi wahanga waliopoteza makazi yao ambapo shule ya msingi Mkondo B imetengwa kuwahudumia wahanga wa kata ya Rudewa na kwa upande wa kata ya Mvumi imetengwa shule ya Msingi Gongwe huku akiongeza kuwa Sérikali inaendelea kutoa huduma nyingine kama vile chakula, Matibabu, Umeme na maji kulingana na uhitaji.
Kwa upande mwingine Mhe Shaka ameishukuru sérikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya wilaya ya Kilosa kiasi cha bilioni 13 kwa ajili ya Ujenzi miundo mbinu Kama vile mitaro na makaravati ambapo imesaidia kutengeneza mmwagiko wa maji kuelekea kwenye mito na kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za mafuriko ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Naye Mbuge wa Jimbo la Kilosa,Profesa Palamagamba Kabudi amewataka Wahandisi wa Barabara na Maji kufanya jitihada za kurekebisha Miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko hayo,huku akizishukuru Taasisi binafsi zilizojitolea kwa namna moja au nyingine kuwasaidia Wahanga wa mafuriko hayo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa