Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Pamoja na LGTI imetoa Mafunzo ya Uibuaji wa fursa na vikwazo ( O & OD ) kwa kutumia mfumo wa MUKI (Mfumo wa ujifunzaji kieletroniki ) kwa Kikosi kazi cha Halmashauri na wawezeshaji ngazi ya msingi kutoka katika kata zote za Wilaya Kilosa lengo likiwa ni kusaidia Serikali katika kutimiza majukumu yake.
Akifungua mafunzo hayo ya siku nne kuanzia Novemba 21 mpaka 24,2023 yanayofanyika katika ukumbi wa MamboyaMjini Kilosa Mgeni Rasmi Ndg Yohana Kasitila ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Idara ya Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI amewataka Watumishi hao kuzingatia mafunzo wanayopatiwa kwani ushiriki wao ni muhimu na kufafanua kuwa mfumo huo utasaidia ushirikishwaji wa jamii katika kuibua Miradi ya maendeleo na kuisaidia Serikali kupunguza gharama.
Amesema kuwa mfumo huo utasaidia kuimarisha Sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi kwa kuwawezesha kufanya maamuzi na kupanga mipango yao wenyewe hivyo amewataka kuzingatia mafunzo kwa kuhakikisha wanaelewa kwa ufasaha Mada zote wanazofundishwa kwani wana jukumu kubwa la kutoa Elimu ya kwa jamii juu ya mfumo huo ili iweze kuibua miradi na kuikamilisha bila kusubiri msaada wa serikali.
Sambamba na hayo Kasitila amewashukuru PS3+, Pamoja na JICA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwezesha na kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika kadri inavyohitajika na kuleta tija kwa jamii ,kwa upande mwingine amewashukuru wadau wote wanaohusika katika jambo hilo.
Kwa upande wake Mhadhiri kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo,Cosmas Maembe ambaye pia ni muwezeshaji wa Mfumo wa fursa na vikwazo amesema kuwa moja ya kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki kikamilifu katika upangaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika ngazi za msingi na Halmashauri na kwamba mafunzo hayo ni muendelezo wa shughuli wanazozifanya .
Amesema kuwa mfumo huo wa ujifinzaji kieletroniki MUKI umekuwa ukitumika katika kutoa mafunzo mbalimbali hata hivyo kwa sasa umeboreshwa zaidi kwaajili ya kuwafanya washiriki waweze kujifunza mahali popote na kuutumia.
Aidha amewasisitiza Washiriki kuhakikisha kuwa wanatumia vyema fursa hiyo adhimu kwani mafunzo wanayoyapata watakwenda kuyatumia katika shughuli zao za kila siku kwani mfumo huo ni rasmi na unatumika kwaajili ya ushirikishaji wa Wananchi kwenye mipango na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa