Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mh. Seleman Jaffo amewataka watendaji wa serikali kutambua nafasi walizopewa na kutambua wajibu wa kila mmoja na kuufanyia kazi kwani wanalo jukumu la kuwahudumia wananchi.
Jaffo amesema hayo wilayani Kilosa Mei 20 mwaka huu wakati wa ziara yake katika kituo cha afya Mikumi na kusema kuwa pamoja na kutumika katika majukumu yao lakini pia amewataka kuwa na usimamizi wa kutosha katika vifaa vinavyonunuliwa viwe katika ubora unaokusudiwa sambamba na kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati.
Aidha ameagiza ujenzi wa kituo hicho uwe umekamilika ifikapo Mei 30 mwaka huu na kwamba tarehe 01/06/219 huduma zianze kutolewa huku akiahidi kuja kutembelea kituo hicho kati ya tarehe 05-12/06/2019 ili kuona huduma zitakazokuwa zikitolewa kwani lengo la Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano ni kuona wananchi wakipata huduma nzuri ikiwemo huduma za kiafya, lakini pia amemuagiza Mganga Mkuu Mkoa kuhakikisha gari la dharura la wagonjwa(ambulance) makao yake makuu yanakuwa katika kituo ili kuwahudumia wananchi wa kawaida wasio na sauti
Pamoja na maagizo hayo Mh Jaffo amepongeza ujenzi wa kituo hicho kwani majengo yake yako vizuri na yanaridhisha yakiwa na ukubwa unaostahiki na kwamba kituo hicho kinapaswa kuwa katika ubora ili kusiwe na hali ya kufanya ukarabati wa mara kwa mara.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe S. Kebwe amemshukuru Waziri wa TAMISEMI kwa ajili gari la dharura la wagonjwa lililoagizwa kuwepo kwenye kituo hicho, wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wamemuahidi Waziri Jaffo kuwa ifikapo Mei 30 kituo hicho kitakuwa kimekamilika na kuanza kazi Juni mosi mwaka huu kama ilivyoagizwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa