Wito umetolewa kwa wafanyakazi wa Umma kujiunga na chama cha TALGWU kwani chama hicho ni muhimu kwa wafanyakazi ambacho ni moja ya sehemu ya kumsaidia mfanyakazi katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kiutumishi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa TALGWU Mkoa wa Morogoro Edmin Mgaya wakati wa ziara ya viongozi wa TALGWU Mkoa katika matawi mbalimbali wilayani Kilosa lengo ikiwa ni kufanya uchaguzi kwenye matawi mbalimbali ya TALGWU sambamba na kusikiliza changamoto mbalimbali za wanachama wa TALGWU.
Mgaya amesema kuwa mojawapo ya kazi zinazofanywa na TALGWU ni kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanachama wake ambapo kwa upande wa madai mbalimbali ya wanachama amesema madai yanayofanyiwa kazi na TALGWU ni yale ambayo yanapelekwa kwao yakiwa na vielelezo, hivyo amewataka wanachama wake kuhakikisha wanakuwa na vielelezo ili waweze kupata usaidizi.
Pamoja na kutoa hamasa ya wafanyakazi kujiunga na TALGWU pia viongozi hao wamesimamia chaguzi mbalimbali zinazoendelea katika matawi mbalimbali wilayani hapa ili kuihakikisha kila tawi linakuwa na uongozi uliokamilika ambapo katika tawi la Boma Peggy Sempemba amepita bila kupingwa kwa nafasi ya Katibu ambapo tawi la Kilimo Theresia Bruno akipita bila kupingwa huku KarimSeleman akichukua nafasi ya mjumbe wa mkoa wa Morogoro kwa wilaya ya Kilosa nafasi ambayo amepita bila kupingwa.
Naye Mwenyekiti wa TALGWU Wilaya Bi. Zena Chacha amewataka wanachama hao kuhamasicha watumishi wengine kujiunga na chama hicho kwani mtu anapokuwa kwenye chama ni rahisi kusaidiwa na kwamba chama hicho ni sehemu sahihi huku akiwataka viongozi wa matawi kuhakikisha wanaitisha vikao ambavyo ni vipo kisheria ili wanachama waweze kufahamu kinachoendelea ikiwemo kusomewa taarifa za mapato na matumizi lakini pia amewataka wanachama hao kuhoji endapo vikao hivyo havifanyiki kila inapohitajika ili viweze kufanyika kwani ni haki yao ya kimsingi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa