Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Abdallah Ulega ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia Desemba 10, 2018 kwa Serikali ya Wilaya ya Kilosa, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kwa kushirikiana na meneja wa Lanchi ya kitaifa ya Mkata iliyopo wilayani Kilosa kuhakikisha inawaondoa wavamizi wa maeneo ya lanchi, wawekezaji wasiolipa kodi pamoja na wawekezaji wanaotumia maeneo ya lanchi kinyume na taratibu.
Ulega amesema kuwa wapo wawekezaji ambao wamepewa maeneo hayo kama wawekezaji lakini wamekuwa wakiyatumia kinyume na matumizi ya maeneo hayo kwa kukodisha ili yatumike kwa kilimo ambapo kiutaratibu eneo la lanchi halipaswi kutumika kwa kilimo, hivyo ameigiza mamlaka husika kuwaondoa mara moja wawekezaji hao kwani wapo ambao wamekuwa wakilikosesha taifa pato kwa kukwepa kulipa kodi kwa ajili ya maeneo hayo na kusisitiza wakati operesheni hiyo ikifanyika ihakikishe haiwahusishi wakulima wasiohusika na kwamba wizara iko tayari kuhakikisha ajenda hiyo inafanikiwa.
Akizungumzia kuhusu mashamba pori amesema wapo watu ambao wanamiliki mashamba makubwa lakini hawayaendelezi hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya na kwamba watu hao wataondoshwa kesho asubuhi Desemba 11, 2018 asubuhi na kwamba katika hilo siasa iweke pembeni hatua zichukuliwe na kwamba mane ohayo ufanyike utaratibu wa kuwapatia watu watakaoyatumia kwa dhati kwa kadri inavyostahiki, sambamba na hayo amemtaka Mkuu wa Wilaya kupitia vyombo vyake vya usalama kuwaondoa watu hao kwani lanchi haitakiwi kulimwa chochote zaidi ya nyasi na kwamba maeneo hayo yanalindwa kwa mujibu wa sheria ya nyanda za malisho na chakula cha malisho na kwamba sheria hiyo ipo kuyalinda maeneo hayo.
Akisoma taarifa yake kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Yuda Mgeni amesema kuwa Wilaya inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe ili kumaliza migogoro wilayani Kilosa ikiwemo kuiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi iwafute wawekezaji waliokodishiwa na kushindwa kuviendeleza vitalu vya NARCO Mkata lanchi vyenye ukubwa wa hekta 16,000, Wizara isaidie kupatikana kwa mitambo ya kuchimba visima virefu 5 na kufukua malambo 7 jambo litakalosaidia kupunguza migogoro kwa kuwa na uhakika wa maji kwa ajili ya mifugo na kuzuia mifugo kuhama hama.
Aidha taarifa hiyo inapendekeza Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Wilaya ifanye tathmini ya athari za kimazingira katika vijiji vilivyotengwa kwa malisho na kuweka mkakati wa pamoja na kurejesha uoto wa malisho, sambamba na kuiomba Wizara katika bajeti yake ya 2019/2020 itenge kiasi cha fedha kusaidia ujenzi wa lambo kubwa katika eneo la Mfilisi, Ihombwe ambalo lina hekta 34,704 ambapo kutekeleza kwa mradi huo kutapunguza migogoro na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Akijibu mapendekezo ya taarifa hiyo Mh. Ulega amesema mapendekezo yaliyotolewa katika taarifa hiyo anayachukua na kuona namna ya kuyafanyia kazi kwa kujadiliana na wizara mbalimbali zinazoonekana kuguswa katika mapendekezo hayo sambamba na kuwataka wafugaji kuwa sehemu ya kuchangia katika kuleta maendeleo katika maeneo yao kwani katika miradi ya maendeleo lazima wananchi wahusike katika kuchangai kujiletea maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa