Wito umetolewa kwa wazazi na jamii kiujumla kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuhakikisha usalama wa watoto kwa kuimarisha ulinzi kwa kuhifadhi chakula cha kutosha ili watoto waweze kukua vizuri na kusoma vizuri kwani elimu ni bure kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari .
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga ambapo amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu bure hivyo kwa kumuunga mkono na kuendana na kaulimbiu ya Mtoto wa Afrika isemayo Tuimarishe Ulinzi wa Watoto, Tokomeza Ukatili Dhidi Yake, Jiandae Kuhesabiwa ni lazima kila jamii ihifadhi chakula cha kutosha mwaka mzima jambo litakalosaidia kuimarisha ulinzi wa mtoto katika chakula na kumfanya mtoto kupata lishe bora ili awe na akili timamu na kuhitimu masomo yake vizuri.
Mwanga amesema kuwa mzazi kushindwa kuhifadhi chakula kwa ajili ya mtoto ni ukatili kama ulivyo ukatili wa aina nyingine hivyo kila mmoja ahahakikishe ulinzi wa mtoto unaimarishwa kwa kuhifadhi chakula cha kutosha na kwamba unapomlinda mtoto ni sawa na kulinda jamii nzima huku akiendelea kusisitiza wananchi kuendelea kujiandaa ili kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi inatyotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya Comrade Shaban Mdoe amesema wazazi bado wana jukumu la kuendelea kutunza na kulinda watoto kwa kuhakikisha haki zote za mtoto zinazingatiwa ikiwemo kupata elimu, malazi, chakula, kupendwa na kusikilizwa huku akitaka wazazi kutohusisha tofauti zao na malezi ya watoto.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Simforosa Mollel akieleza mambo yaliyobebwa katika ujumbe wa siku ya Mtoto wa Afrika amesema kila mzazi anao wajibu wa kufahamu mwenendo wa mtoto na kuwalinda dhidi ya ukatili unaoweza kutokea dhidi ya vitendo viovu pamoja na kuhakikisha watoto wanashiriki katika zoezi la sensa kwa kuhesabiwa kwa ajili ya kuwezesha uchumi na mipango ya Taifa.
Wakisoma risala yao watoto hao wameishkuru Serikali ya aawamu ya sita kwa kuwapatia elimu bure isiyo na vikwazo kwa kujenga na kuboresha vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, vyoo, maabara ya masomo ya sayansi, mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume pamoja na maktaba huku wakiiomba Serikali na mashirika binafsi kuwajengea miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, kuboreshewa mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ufadhili kwa watoto wanaoishi mazingira magumu na hatarishi na huduma ya chakula mashuleni, wazazi wasiotekeleza majukumu yao wachukuliwe hatua pamoja na kuwafatilia wahusika wanaowapa wanafunzi mimba.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa