Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wametakiwa kuimarisha mfumo wa malezi kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu bila kubagua makundi ya watoto wenye mahitaji maalumu ili kutengeneza kizazi bora chenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa Juni 16, 2024 na Afisa Tawala kutoka Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kilosa Angela Mono wakati akihutubia kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Shaka Hamdu Shaka katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambazo Kiwilaya zimefanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Zombo katika kata ya Zombo.
Bi. Mono amesema kuwa kutokana na ripoti mbalimbali kuonesha baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania kukabiliwa na changamoto ya watoto wenye mahitaji maalum kukosa haki ya elimu au kuipata wakiwa katika mazingira yasiyo rafiki kwa hali walizonano, serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabili changamoto hizo.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutunga Sera ya Elimu Jumuishi kwa watoto ambapo kutokana na sera hii hatua kadha zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwahusisha wadau na mashirika mbalimbali katika elimu, ujenzi wa miundombinu rafiki, kutoa mafunzo kwa walimu pamoja na kuandaa kampeni mbalimbali za elimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashari ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred Sumari ameitaka jamii kuboresha huduma za lishe kwa watoto ili kuimarisha afya ya mwili na akili za watoto.
Aidha amewetaka wananchi kuiunga mkono serikali kwa kuwapeleka watoto shule ikiwa ni pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu ikiwa kama vile kuwapatia huduma za afya kwani serikali ya awamu ya sita imeboresha miundombinu ya elimu na afya.
Naye mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Alto Mbikiye akiifafanua kaulimbiu ya maadhimisho hayo, ameishauri jamii kujenga kizazi chenye maarifa pamoja na stadi mbalimbali za kazi ili ziwasaidie kujiepusha na matendo yasiyo mema kwenye jamii.
Hata hivyo, amewashauri wazazi kuwa waangalizi kwa watoto wao katika matumizi ya vifaa vya TEHAMA kama vile kompyuta na simu kwani wanaweza kukumbana na maudhui yasiyofaa kutokana na kukua kwa utandawazi.
Akitoa salamu katika maadhimisho hayo, diwani wa kata ya Zombo, Mhe. Lusinde Elias ameishukuru serikali ya wilaya kuadhimisha sherehe hizo kwenye kata yake na kuwataka wananchi wake kudumisha malezi bora kwa watoto wao.
Maadhimisho haya yanabebwa na kaulimbiu isemayo; Elimu Jumuishi Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa