Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya msaada wa kisheria unaotolewa bure kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia ili waweze kuzijua haki zao lakini pia kuepuka migogoro mbalimbali inayokwamisha maendeleo.
Mhe. Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo katika sherehe za uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria zilizofanyika Disemba 15, 2024 katika kata ya Magomeni.
Waziri Ndumbaro amefafanua kuwa iwapo misingi ya Usawa, Haki na Amani itadumishwa, itasaidia kuleta maendeleo kwenye jamii kwani misingi hiyo itasaidia kupunguza migogoro kwenye jamii.
Aidha amesema kuwa kampeni hii ambayo itadumu kwa siku kumi, inalenga kumaliza migogoro mbalimbali hususani migogoro ya wakulima na wafugaji na kuongeza kuwa baada ya kampeni hii, itaandaliwa ripoti ili kubainisha migogoro ambayo haijaisha ili uwekwe utaratibu maalumu wa kuimaliza migogoro hiyo.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuileta huduma hii karibu na wananchi hususani wale wasioweza kumudu gharama za kuwaajiri wanasheria pale wanapohitaji huduma za kisheria.
Aidha Mhe. Prof. Kabudi amewataka wakazi wa Kilosa kujitokeza kwa wingi kupata huduma hii ambayo itatolewa kwa siku kumi kwenye vituo tofauti tofauti.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujifunza masuala ya kisheria katika vituo vilivyotengwa ili kuepusha wimbi la watu wanaokwenda kwenye ofisi zisizo rasmi katika kutatua migogoro hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameipongeza serikali kwa kuileta huduma hii kwani itasaidia kupunguza migogoro inayoikumba jamii huku akiitaja migogoro ya ardhi pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji kuwa kero ndani ya wilaya ya Kilosa.
Aidha, Mhe. Shaka ameiomba serikali kuongeza muda wa kutoa huduma hii lakini pia kuongeza vituo vya kutolea huduma hii ili kukidhi mahitaji ya wilaya kutokana na ukubwa na mahitaji, siku za ziada zinahitajika.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa