Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kufikia mwezi Disemba mwaka huu iwe imejenga wodi mbili za magonjwa mchanganyiko zisizo na gharama kubwa kwa kinamama na kinababa katika kituo cha Afya Mikumi ili wananchi waweze kupata huduma stahiki badala ya kusafiri kwenda hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro.
Majaliwa ametoa maagizo hayo Septemba 17 mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku moja ya ambapo pia ametaka kuwepo kwa chumba cha upasuaji ambacho wananchi watapata huduma zote badala ya kwenda Morogoro kupata huduma kubwa za upasuaji ikiwemo upasuaji kwa ajili ya kinamama wakati wa kujifungua lakini pia ametaka huduma zote muhimu za kitabibu kupatikana katika kituo cha afya cha Mikumi na Malolo ambako ujenzi unaendelea.
Akizungumzia upande wa Hospitali ya Kilosa amesema serikali itaendelea kuimarisha hospitali hiyo huku hospitali za wilaya zikiendelea kujengwa katika wilaya zisizo na hospitali za wilaya mkoani Morogoro ambapo amesema serikali imeanza kuajiri wataalam wa afya wakiwemo madaktari ili waweze kutoa huduma huku akitoa onyo kwa madaktari kutowaandikia wagonjwa kununua dawa katika maduka ya dawa ya nje ya hospitali kwani serikali ya awamu ya tano imejiimarisha vema katika sekta ya afya kwa kuhakikisha inatoa huduma stahiki.
Sambamba na hayo amewataka watumishi wa Umma kutocheza na fedha za serikali kwani fedha hizo ni kwa ajili ya kuwaletea maendeleo ya wananchi na kwamba fedha hizo ni za moto, hivyo zitumike kwa kadri zilivyopangwa lakini pia ameagiza walimu kutochangisha wazazi michango kiholela na kwamba suala la uchangishaji michango liko chini ya dhamana ya Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye msimamizi mkuu.
Aidha ameagiza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa kata ya Ruaha kwa kuchimba kwa visima vifupi vya maji ikiwa ni sehemu ya ufumbuzi wa kero ya maji huku akisisitiza kutimizwa kwa ahadi mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa huduma ya maji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa