Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo kutoa tamko la kisera la zuio la uwepo wa matumizi ya kamba za plastiki nchini katika kufungashia mazao mbalimbali.
Agizo hilo limetolewa Septemba 13 mwaka huu Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro katika Mkutano wa pili wa wadau wa sekta ya Mkonge lililosomwa kupitia hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe ambapo amesema ili kuimarisha masoko ya ndani ni muhimu sana hivyo ni lazima kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika viwanda vya uongezaji mnyororo wa thamani wa zao la mkonge ili kuliendeleza zao hilo.
Aidha ameiagiza Wizara ya kilimo, bodi ya Mkonge, kituo cha utafiti Tari Mlingano na Halmashauri za Wilaya zinazolima zao hilo kuhakikisha wanafanya kazi kama timu ili kuleta mapinduzi katika zao la Mkonge nchini huku akisema lengo la Serikali katika kuongeza uzalishaji kutoka tani 37,000 zilizozalishwa kwa mwaka hadi kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2025 ambapo amesema kuwa mijadala yao inapaswa kujikita katika kuboresha tija katika zao la Mkonge.
Aidha amewataka kuhakikisha wanawasaidia wakulima wadogo kutumia mbinu za kilimo bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanasaidiwa kumudu utunzaji wa mashamba ili wamudu kutumia eneo dogo kwa mavuno makubwa ikiwa ni pamoja na kupatiwa mafunzo ya ugani na kuzingatia utimilivu wa idadi ya miche kwa eneo.
“hatuwezi kuongeza tija wala kufanikiwa katika kilimo cha mkonge ikiwa hakuna maeneo ya kulima zao hilo”amesema
Waziri Mkuu ameitaka bodi ya mkonge kuharakisha mchakato wa ugawaji mashamba ili wananchi wengi waweze kupata mashamba ya kulima mkonge na kwamba bodi hiyo isiishie kugawa pekee lakini pia ihakikishe wakulima wote wanalima na kupanda kwa wakati mmoja na kuwaunganisha na wanunuzi huku akiitaka kuhakikisha inashirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya zinazofaa kwa kilimo cha zao hilo kutenga ardhi za kilimo hicho kwa wakulima wadogo, wakubwa na wawekezaji na kwamba wanapogawa mashamba yaliyorudi kuyagawa kwa wakulima wadogo pamoja na wawekezaji wapewe mashamba kwa masharti ya kulima mkonge.
Mh.Bashe ameiagiza bodi ya mkonge ya kuwa na ofisi katika wilaya ya Kilosa lakini pia vitalu kwa ajili ya kuzalisha miche watakayowapatia wakulima pindi itakapokuwa tayari huku akiipiga marufuku NFRA kununua kamba za plastiki kwa ajili ya kufungia magunia badala yake wanunue kamba za katani na kwamba gunia za katani ndizo zitatumika hivyo tenda yoyote itakayohitaji vifungashio kipaumbele kitakuwa katika magunia ya katani na Wilaya ya Kilosa itapata sapoti ya kutosha ili kukuza zao la mkonge.
Wakieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika zao la mkonge Mwenyekiti wa wadau wa zao la mkonge Damian Luhinda na Mwenyekiti wa bodi ya mkonge Bi Mariam Mkumbi wamesema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo ni ukosefu wa mitaji, ushindani wa bidhaa za plastiki, kuongezeka kwa gharama za mashamba(kodi), uvamizi wa tembo mashambani na matumizi makubwa ya kamba bandia ambazo ni tofauti na kamba za mkonge pamoja na tembo ambao wamekuwa wakiharibu zao la mkonge likiwa lingali shambani na kusababisha hasara kwa wakulima hivyo wameiomba Serikali kudhibiti uzalishwaji na matumizi ya kamba bandia kwani uwepo wa matumizi ya kamba bandia unaua soko la kamba stahiki lakini pia wameiomba Serikali kudhibiti vurugu zinazofanywa na tembo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa