Julai 22 mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amewataka wenyeviti wa vijiji vyote na watendaji wa vijiji vinavyohusika na uvunaji mazao ya misitu kama vile kuni, mbao na mkaa kuwa wasimamizi wazuri wa rasilimali za misitu kwani kumekuwa na uvunaji holela usiozingatia sheria, kanuni na taratibu na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Mgoyi amesema hayo katika kikao cha kamati ya uvunaji wa mazao ya misitu ambapo amesema kuwa wavunaji wengi wamekuwa wakivuna chini ya usimamizi mdogo wa wenyeviti wa vijiji na watendaji na kupelekea uhujumu uchumi katika uvunaji mazao ya misitu ambao utapelekea Wilaya ya Kilosa kuwa jangwa.
Aidha amesema kuwa wenyeviti na watendaji wanapaswa kusimamia na kuhakikisha uvunaji unafanyika inavyostahiki ili kulinda misitu kwa ajili ya vizazi vijavyo ambapo amebainisha kuwa upande wa Kaskazini mwa Kilosa hasa kijiji cha Makwambe hali ya uvunaji misitu si nzuri na kwamba endapo hali ya uvunaji holela ikiendelea vibali vya uvunaji vitasitishwa ili kuepusha hali ya wilaya kuwa jangwa.
Mgoyi katika kikao hicho amewakumbusha wenyeviti wa vijiji na watendaji kuwa na kumbukumbu za shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu huku akisisitiza kuwepo kwa daftari la kumbukumbu za uvunaji wa mazao ya misitu jambo litakalosaidia utunzaji kumbukumbu sambamba na watendaji wa idara ya maliasili na TFS kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika majukumu yake ya usimamizi na kutekeleza maazimio yanayoamriwa katika vikao.
Aidha katika kikao hicho amekemea vikali uzembe ambao umekuwa ukifanyika wa kutosimamia vema na kutekeleza maazimio yanayotolewa katika kikao kwani maazimio yaliyoazimiwa hayajafanyiwa kazi na kuisababishia hasara serikali ikiwemo kutolipa kodi ama michango stahiki ya mazao ya misitu na kwamba wavunaji wote wenye madeni hawataruhusiwa kuendelea kuvuna hadi watakapomaliza madeni na kuwa hatua stahiki zitachukuliwa kwa wote wasiolipa madeni ikiwemo kutoa matangazo kwa umma ya kutoruhusiwa kupata kibali eneo lolote kwa ajili ya uvunaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa