Wenyeviti wa vijiji wametakiwa kuiga mfano wa utendaji kazi wa Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano namna anavyowajibika na kujituma ambayo ni dira na mwelekeo kwa viongozi hao hivyo kila mmoja awajibike kwa nafasi yake na kuachana na hulka ya kuchongeana kwa lengo ovu la uchochezi pindi wanapotembelewa na viongozi badala yake kila mmoja awajibike kwa sehemu yake kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi ambao wamewapa ridhaa ya kuwaongoza.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa rai hiyo Januari 8 mwaka huu wakati wa mafunzo kwa wenyeviti wa vijiji ambapo amesema kuwa katika utawala huu viongozi hao wanapaswa kutambua kuwa wanao wajibu mkubwa wa ambaye hatawajibika ipasavyo hatavumiliwa kwani kinachotakiwa ni uwajibikaji na utawala bora katika kuiendesha serikali katika vijiji vyao kwa kuhakikisha wanafanya majukumu yao ipasavyo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Aidha amewataka viongozi hao kuacha uchu wa madaraka kwa kutaka kuwa viongozi katika kila kamati zilizopo katika vijiji huku akisisitiza kuitishwa kwa vikao vya kisheria na kusoma taarifa za mapato na matumizi na kwamba kiongozi yoyote ambaye hatasoma taarifa kwa vikao vitatu mfululizo hafai kuendelea kuwa kiongozi kwani kwa kutokusoma taarifa kunaibua migogoro na kwa kiongozi yoyote ambaye hataitisha vikao na kusoma taarifa za mapato na matumizi hatavumiliwa na kuondolewa mara moja katika nafasi hiyo, lakini pia ametoa onyo kwa viongozi hao kutoingilia majukumu ya watu wanaofanya nao kazi kwani wajibu wao ni kusimamia na kuhakikisha mambo yote waliyojiwekea yanafanyika ipasavyo na taratibu zinafuatwa.
Sambamba na hayo amewataka viongozi hao kutatua kero katika vijiji vyao kwa kufuata ngazi kwa ngazi ikiwemo kuachana na hulka ya kuruka ngazi na kupeleka kero hizo kwa viongozi wa juu pasipo kushirikisha viongozi wa kata, Wilaya na wakati mwingine hata uongozi wa mkoa ambapo licha ya kuruka ngazi bado kero hizo zitarudishwa katika ngazi husika kwani serikali hairuki hatua ilizojiwekea kwa kukasimu madaraka katika mgawanyiko unaofuata sheria na taratibu huku akisistiza kutambua kuwa viongozi walio juu yao kuwa ni watu kama wengine na wana haki zao zinazopaswa kulindwa.
Licha ya hayo amewataka wenyeviti hao kuwa mstari wa mbele katika shughuli za elimu kwa kuhakikisha walimu walioko katika shule zilizopo katika vijiji vyao wanakuwa katika mazingira mazuri, wanafundisha inavyostahiki huku wazazi wakihusika kikamilifu katika kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa chakula mashuleni kwa ajili ya watoto ambao ni kizazi chao ambapo pia ametaka kila mwaka vijiji vinakuwa na akiba ya tofari ambazo ni msaada mkubwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, ofisi na zahanati katika vijiji.
Naye mkuu wa TAKUKURU Wilaya Lawrance Mlaponi amewataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanazuia vitendo vya rushwa ambayo mara nyingi hujitokeza unapotokea mgongano wa kimaslahi ikiwemo upangaji wa matumizi yasiyo na maslahi kwa wananchi pamoja na kutosoma taarifa za mapato kunakotokana na kufanya matumizi yasiyo sahihi ambayo yanazaa maswali kwa wananchi na kuleta sintofahamu itokanayo na kukosa ukweli na uwazi ambapo pia amewataka kuhakikisha kila mwezi serikali ya kijiji inakaa na kujadili utendaji wa serikali katika kijiji kwa lengo la kutekeleza waliyojipangia ili kuleta maendeleo huku akisistiza kutojihusisha na maslahi binafsi ikiwemo kujihusisha katika ubadhirilfu wa vyanzo vya mapato kwa namna yoyote ile.
Mlaponi amesisitiza kufuatwa kwa taratibu, sheria na kanuni ambapo amesema kuwa viongozi hao wanapaswa kuhakikisha wanasoma taarifa za mapato na matumizi ambapo pia kutambua kuwa wanao wajibu wa kuwasimamia watendaji wa vijiji, kusimamia ukusanyaji wa mapato na kukemea vikali tabia ya uchezeaji wa mashine za kukusanyia mapato POS kwani imezuka tabia ya kuzichezea mashine hizo kwa lengo la kujipatia kipato kwa njia za ubadhirifu jambo ambalo ni kosa kisheria na yoyote atakayebainika kushiriki katika mchezo huo serikali kupitia TAKUKURU haitasita kumchukulia hatua kwa kumfikisha katika vyombo vya dola kwa hatua zaidi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa