Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga amewasimamisha kazi wenyeviti wa vitongoji watatu kwa makosa mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka
Mwanga amechukua hatua ya kuwasimamisha wenyeviti hao na kuwaondoa madarakani kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuuza maeneo ya hifadhi ya misitu zaidi ya hekari 70 pamoja na mashamba ya wananchi kwa wafugaji kinyume cha sheria ya ardhi.
Akiwataja wenyeviti hao walioondolewa kwa makosa hayo ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Masugu Kati Kondo Pilipili, kitongoji cha Masugu John Kalonga na Ally Liguta kitongoji cha Mitalulani.
Katika hatua nyingine amemtaka mtendaji wa kijiji cha Dodoma Isanga Andrew Kazimbaya kuripoti katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ili apangiwe majukumu mengine kwa kushindwa kusimamia majukumu yake katika kijiji hicho, huku akiwaagiza wataalam wa kata ya Magomeni akiwemo Mtendaji wa kata, Afisa Maendeleo ya jamii, Afisa Mifugo na Afisa Kilimo kuandaa taarifa ya kina juu ya migogoro iliyosababishwa na wenyeviti hao na kuiwasilisha ofisi ya Mkuu wa Wilaya ndani ya siku saba.
Aidha amewataka wananchi kujitokeza kwenye ukusanyaji wa taarifa za Anwani za Makazi na Postikodi zoezi linaloendelea kwasasa, sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti pamoja na kupata kinga ya uviko - 19 huku akisisitiza kuanza mara moja ujenzi wa shule shikizi ili kuondoa adha wanayopata wanafunzi kwa kutembea umbali mrefu na nyakati za mvua.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa