Katika kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani na Siku Ya upandaji Miti Kitaifa, Wilaya ya Kilosa leo Machi 22,2025 imefanikisha tukio la kihistoria kwa kupanda Miti elfu mbili katika Shule ya Sekondari Mazinyungu, ikiwa ni sehemu ya Juhudi za Serikali kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa misitu na utunzaji wa mazingira.
Afisa Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wilaya ya Kilosa, Hamis Nzunda, amewahimiza wananchi kuendelea kushiriki katika juhudi za kupanda miti ili kufikia lengo la serikali la kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri ifikapo mwaka 2025.
“Leo tumepanda miti elfu mbili, lakini kazi bado ni kubwa,tutashirikiana na wadau wengine kuhakikisha tunafikia malengo yetu na kufanya Kilosa kuwa mfano wa utunzaji wa mazingira,” alisema Nzunda.
Naye Afisa kutoka Mamlaka ya Misitu Tanzania (TFS), Hilda Mwalongo amesema sherehe hizo huadhimishwa kila Mwaka Tarehe 21,Machi ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhamasisha wananchi kuhusu faida ya misitu na umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kwamba ushirikiano baina ya TFS na Serikali na mzuri katika utunzaji wa mazingira na kusema kuwa wametoa miche elfu mbili kwa jamii ya kwaajili ya kufanikisha Zoezi hilo katika Wilaya ya Kilosa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi, ameitaka jamii kuhakikisha wanajitolea kutunza miti ili kuweza kupata manufaa ya mazingira, huku akiwasisitiza Wananchi kuiunga mkono kwa vitendo Kaulimbiu ya mwaka huu 2025 isemayo” Ongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Kizazi cha Sasa na Kijacho”
“Misitu ni Rasilimali muhimu kwa ustawi wa jamii na ikiwa hatutahakikisha tunalinda misitu yetu, tutakuwa na athari kubwa za mazingira kama ukame na mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema Kabudi, akiongeza kuwa jamii lazima itambue faida zinazopatikana kwa kuendelea kutunza mazingira.
Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, amewapongeza Wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika juhudi za kupanda miti, akisema kuwa Misitu ni biashara inayoweza kuleta maendeleo kwa jamii.
“Mabadiliko ya hali ya hewa na uhaba wa rasilimali ni changamoto kubwa. Misitu ni biashara, na uvunaji wa hewa mkaa na mazao mengine ya misitu inaweza kuwa chanzo cha mapato kwa wananchi wa Kilosa na wananchi wanapaswa kutambua kuwa utunzaji wa misitu ni uwekezaji wa baadaye kwa vizazi vijavyo,” alisisitiza Shaka.
Kwa upande mwingine, Wananchi wameishukuru Serikali kwa kuanzisha shughuli hiyo ya kupanda Miti na kuhamasisha umma kuhusu kutunza mazingira na kwamba elimu waliyopata itawawezesha kuwa na uelewa mkubwa wa faida za misitu na jinsi ya kuitunza ili iweze kutoa huduma endelevu kwa jamii.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa