Imeelezwa kuwa Wizara ya Uchukuzi imefanyia kazi Mpango wa kuhakikisha inawezesha Taasisi zake na Sekta za Usafirishaji kwa ujumla kupata mizigo ya uhakika itakayowezesha Taasisi hizo na Sekta mbalimbali kufanya biashara na kutoa matokeo chanya.
Hayo yameelezwa Oktoba Mosi 2024 na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile kwa niaba ya Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa upatikanaji wa mizigo ili kuimarisha biashara ya usafirishaji nchini.
Mhe. Kihenzile ameitaka Wizara ya Uchukuzi kusimamia mambo matano ili kuongeza ufanisi wa Mpango huo kuendelea kufanya vizuri na kufikia malengo yake ambapo mambo hayo ni kubainisha mahitaji ya suluhisho la uhakika la usafiri katika njia ya ubaridi kutoka shambani hadi sokoni ili kuzuia uharibifu baada ya kuvuna, kutoa mafunzo kwa Wakulima wadogo kuhusu Kilimo bora na utunzaji wa mazao baada ya kuvuna, kushirikiana na Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ili kurahisisha utekelezaji wa suluhisho la usafirishaji kwa njia ya ubaridi, kuunda vikundi vya Wakulima na Wafanyabiashara ili kuongeza tija ya ukusanyaji wa mazao yao na uhakika wa upatikanaji wa masoko pia kufanya tafiti Zaidi ya hasara baada ya mavuno na hatua za kupunguza changamoto hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa amesema kuwa Wakulima wa mbogamboga wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo kwani itakuwa ni suluhisho kubwa la kuwapunguzia gharama za usafirishaji wa bidhaa hizo na pia itawasaidia kujipatia kipato.
Aidha kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameishukuru timu ya utafiti iliyofanya utafiti huo na kusema kuwa kwa upande wa Kilosa asilimia 82 ya wananchi wanajishughulisha na kilimo,ambapo kati yao asilimia 45 wanafanya Kilimo cha Mboga mboga hivyo mpango huo utaleta matokeo chanya.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa